November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CBE kuwakutanisha wanataaluma Dodoma

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kufungua mkutano wa Tano wa Biashara na Maendeleo ya Kiuchumi (BEDC) 2024) ambao umeandaliwa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) utakaofanyika kuanzia Novemba 22,mwaka huu mkoani Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa chuo cha CBE, Profesa Edda Lwoga, alisema lengo la mkutano huo ni kujadiliana kuhusu masuala muhimu yanayohusu biashara na maendeleo ya kiuchumi.

Amesema mkutano kama huo ulianzishwa mwaka 2020, na tangu wakati huo umejidhihirisha kuwa jukwaa muhimu la mijadala ya kibiashara na kiuchumi, likiwakutanisha washiriki kutoka sehemu mbalimbali za Dunia.

“Lengo kuu la mkutano wa tano wa Biashara na Maendeleo ya Kiuchumi (BEDC 2024) ni kuwaleta pamoja wataalamu, wajasiriamali, watafiti, na wadau wa maendeleo kutoka sehemu mbalimbali za Dunia kujadili masuala muhimu ya biashara na maendeleo ya kiuchumi,” amesema na kuongeza:

“Mkutano huu utajadili mbinu za kukuza biashara, masuala ya uwekezaji, uvumbuzi, maendeleo endelevu, na changamoto za kiuchumi, huku ukitoa fursa ya kubadilishana mawazo, kujifunza, na kujenga mtandao wa kitaalamu kwa ajili ya maendeleo ya uchumi wa dunia,” amesema.

Amesema mkutano huo unatoa fursa muhimu kwa washiriki kupata maarifa mapya, kujenga mitandao ya kitaalamu, na kuchangia katika maendeleo endelevu ya biashara na uchumi duniani.

“Tunakaribisha wataalamu, wajasiriamali, na wadau wa maendeleo kushiriki katika mkutano huu ili kujadiliana na kuboresha sekta mbalimbali za uchumi na biashara duniani,” amesema.

Amesema makongamano hayo yalianza mwaka 2016 mara baada ya serikali kutangaza kuhamia Dodoma na baadaye yakageuka kuwa mikutano ya kitaaluma, yakilenga kuimarisha mijadala na tafiti zinazohusu biashara na maendeleo ya kiuchumi.

Amesema mikutano hiyo imekuwa ikikusanya wataalamu, wafanyabiashara, na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi ili kujadili na kubadilishana mawazo, kutoa mapendekezo, na kuhamasisha ushirikiano kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Amesema tangu mwaka 2020, Chuo kimeandaa mikutano minne ya kitaaluma, ambayo yote imelenga kuunga mkono juhudi za serikali za kukuza fursa za biashara na uwekezaji nchini.

Amesema katika mkutano wa BEDC wa mwaka 2022/2023, jumla ya machapisho 169 na matokeo ya tafiti ziliwasilishwa na watafiti kutoka ndani na nje ya nchi na kujadiliwa na wataalamu mahiri katika fani mbalimbali.

Amesema mawasilisho katika Kongamano hilo yatajikita katika mada ndogo ambazo zitajadiliwa baada ya ufunguzi na mawasilisho ya wasemaji muhimu na kwamba mwaka huu CBE inatarajia kutakuwa na machapisho zaidi ya 170 yatakayolenga katika mada ndogo saba na kwamba watoa mada wanaotarajiwa wanatoka nchi za Afrika Mashariki, Ethiopia, na China.

Ametaja malengo makuu ya mkutano wa mwaka huu kuwa ni pamoja na kujenga uwezo na mitandao, kukuza maarifa, kuunda mitandao, fursa za kibiashara, kutangaza kazi za wataalamu na fursa za maendeleo ya kiuchumi.