Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online, Handeni
WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso amesema ili kumaliza tatizo la maji kwenye Kijiji cha Msomera, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga ni kujenga bwawa la kimkakati lenye ukubwa wa ziwa, ambalo litasaidia wananchi na mifugo wote kupata maji kwa urahisi.
Amesema bwawa hilo watajenga kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Maji, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, hivyo anakwenda kukutana na wahusika wa wizara hizo ili kukubaliana kwa jambo hilo la kudumu.
Ameyasema hayo Machi 9, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Msomera mara baada ya kumaliza kukagua miradi ya maji ikiwemo bwawa kwenye maeneo ya kijiji hicho ambacho wananchi wamefikia zaidi ya 6,000.
Amesema nchi inapata mvua nyingi kila mwaka,maji yake yanakwenda baharini kama watajenga bwawa kubwa la kimkakati, wataweza kumaliza kabisa tatizo la maji kwenye Kijiji cha Msomera.
“Wazo lenu la kutaka kupata maji kutoka Mto Pangani nimelichukua, na nitampelekea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini ni gharama kubwa, itabidi hata mifugo iwekewe mita kwa ajili ya kunywa maji kwa vile shida yenu ni maji, acha sisi Serikali tuwawekee maji ambayo yatakuwa ni rahisi kuyatumia,” amesema Aweso.
Aweso katika kuweka msisitizo amezitaka taasisi zote zilizopo chini ya Wizara ya Maji kuanzia Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA), Bonde la Pangani, na Mamlaka ya Majisafi Handeni Trunk Main (HTM), wataalamu wake kubaki Msomera ili kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa mipango ya muda mfupi, wa kati na mrefu.
Aweso amesema kwenye ziara ya kukagua miradi ya maji, amejiridhisha kwa kazi zilizofanyika, kwani visima vingi vilivyochimbwa kwenye kijiji hicho vinatoa maji na kuwapongeza RUWASA na wataalamu wengine kwa kazi nzuri, hivyo watafanya jitihada maji hayo yawafikie wananchi kwa njia ya bomba.
“Ametupitisha (Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga, Mhandisi Upendo Lugongo), na kuona kazi nzuri iliyofanyika ya kuchimba visima. Visima vingi vilivyochimbwa baadhi yao vinatoa maji mengi, lakini niwaambie, pamoja na visima hivyo kutoa maji, wananchi hawataki visima bali wanataka maji kwa haraka sana, tutahakikisha tunaweka pampu za kuvuta maji hayo na yawafikie wananchi, huku Mkandarasi akijenga matenki ili wananchi wote wapate maji safi,”amesema Aweso na kuongeza kuwa
“Lakini pia tumeweza kutembelea bwawa letu kazi kubwa imefanyika, tumeona ujenzi wake umefikia asilimia 75. Tumemtaka Mkandarasi kuanzia Jumatatu (Machi 11) aongeze timu na kasi zaidi ya ufanyaji kazi ili wananchi wa Msomera wapate maji na mifugo yao isiweze kuteseka” amesema Aweso.
Aweso amesema Serikali imetoa fedha nyingi ili kujenga miundombinu ya maji, hivyo amewataka wananchi wamuunge mkono Rais Dkt. Samia kwa kutoharibu miundombinu hiyo ya maji, aidha kwa kukata mabomba ama hujuma nyingine, huku akiwasisitiza wananchi wawe na subira kwani maji yatafika kwenye maeneo yote ya Msomera.
Mbunge wa Jinbo la Handeni Vijijini John Sallu amesema Wizara ya Maji inafanya kazi kubwa kuona maji ya bomba yanakuwepo Msomera, hivyo wataendelea kuwa wavumilivu wakati huu kuona wananchi wote wanapata maji.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Wakili Albert Msando amesema jitihada za Serikali kwa ajili ya kufikisha huduma za jamii ikiwemo maji zinaendelea, na yeye ameweka makazi kwenye kijiji hicho kuona mambo yanakwenda sawa.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam