September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Butiku ataka jitihada za Samia ziungwe mkono

Na Jackline Martin,Timesmajiraoline,Dar

TAASISI ya Mwalimu Nyerere imewataka Watanzania kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kukomesha tabia mbaya zilizozuka nchini kuteka, kunyanyasa na kuua Watanzania.

Rai hiyo ilitolewa na Mwenyekiti Bodi ya Wadhamini Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kile alichokiita tabia mbaya zinazohatarisha usalama wa maisha ya Watanzania na mali zao

“Tunaye Rais mmoja tu sio wawili wala watatu tuliye mkabidhi Katiba ya nchi yetu ili aitumie kuongoza Taifa letu na kuhakikisha usalama wa Watanzania wote na wageni wanaoingia katika Taifa letu na pia kulinda mali zetu. Huu ni wajibu wa Kikatiba wa Rais wetu anautekeleza kwa niaba yetu tumuunge mkono bila maswali.” Alisema.

Aidha, aliwaomba Watanzania na viongozi kukubali kwamba Taifa la Tanzania si la wauaji wala la wahuni, bali ni Taifa la watu wanaoishi kwa kuzingatia Katiba ya nchi na sheria zinazotokana na Katiba hiyo.

“Sisi sote tunao wajibu wa kufuata na kutii Katiba yetu na sheria zote zinazotokana Katiba hiyo, na ambazo hazikiuki Katiba. Hakuna nafasi wala ruhusa kwa raia yeyote wa nchi hii kuishi nje ya utaratibu huu. Huu ndio msingi wa amani, umoja, na maendeleo yanayo shirikisha wananchi wote kwa faida yao.

Kwa maana hii, sisi Watanzania ni wastaarabu. Tusiseme hatuwajui wahalifu hao, tunawajua. Wanaishi miongoni mwetu katika kaya zetu, wako ndani ya vyombo vyetu vya dola, wako makanisani na katika misikiti. Tunawajua, lazima Serikali yetu iwajue,” alisisitiza Butiku na kuongeza;

“Kwa hiyo Taasisi ya Mwalimu Nyerere inaomba tumsaidie Rais kupata
taarifa sahihi kuhusu wabaya wetu hao ili achukue hatua stahiki. Anavyo vyombo vya dola vyenye majukumu mahsusi ya kumpa taarifa za uhakika.

Nchi yetu imeviwezesha kuwa na uwezo wa kutosha wa utaalamu na nyenzo za kazi. Viongozi wa vyombo hivi wasituambie kwamba hawajui, wanajua. Wasituambie kwamba wanamuogopa Rais, wasimsingizie.”

Jumapili wiki iliyopita mara baada ya kada wa CHADEMA na mjumbe wa Sekretarieti ya Taifa, Ali Kibao, mwili kupatikana umeuawa baada ya kutekwa Septemba 6, mwaka huu Rais Samia, aliagiza vyombo vya uchunguzi kumpelekea taarifa ya mauaji ya kioogozi huyo.

Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa Septemba 8,2024 katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii alitoa maelekezo hayo akieleza kusikitishwa kwa tukio hilo.

“Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya mauaji ya kiongozi wa CHADEMA, bwana Mohamed Ali Kibao. Natoa pole kwa viongozi wa chama hicho, familia ya Mzee Kibao, ndugu, jamaa na marafiki,”

“Nimeagiza vyombo vya uchunguzi kuniletea taarifa ya kina kuhusu tukio hili baya kabisa na mengine ya namna hii haraka. Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi. Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii,”.alisema Rais Samia

Juzi Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mhandisi Hamad Massaun, alisema maelekezo ya Rais Dkt. Samia yameshaanza kutekelezwa na hatua zitachukuliwa kwa wale watakaobainika kuhusika na tukio la mauaji ya Kibao.

Masauni alitoa kauli hiyo wakati akiwasilisha salamu za Serikali katika mzishi Kibao yaliyofanyika nyumbani kwake mkoani Tanga. “Nimekuja hapa kuwapa salamu za Serikali kupitia viongozi Wakuu akiwemo Rais Samia ambaye ameonesha kuguswa na tukio hilo, na maelekezo aliyoyatoa ili kuweza kufanywa uchunguzi kwa haraka hatimaye wahusika wote waweze kuchukuliwa hatuna kwa mujibu wa sheria,” alisema na kuongeza;

“Rais amesononeshwa, amesikitishwa na ameumizwa sana na tukio hili pamoja na Serikali nzima ni jambo ambalo halikupaswa kutokea hasa katika nchi yetu ambayo kwa miaka yote tumekuwa tukijivunia juu ya usalama na amani ya nchi hii na mfano bora ukilinganisha na nchi zingine zinazotuzunguka Duniani,” alisema Masauni.

Kibao, aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema alichukuliwa jioni ya Septemba 6, 2024 eneo ya Kibo Complex Tegeta jijini Dar es Salaam na watu wasiojulikana, akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea Tanga na basi la Tashriff na mwili wake kupatikana jana Jumapili Septemba 8, 2024 eneo la Ununio, Dar es Salaam.