Ashura Jumapili TimesMajira Online,Bukoba
Maambukizi ya bungua mweusi wa zao la Kahawa yameendelea kusambaa katika maeneo mengi mkoani Kagera,hivyo yanaweza kushusha uchumi wa Mkoa hasa Wilaya ya Bukoba.
Kauli hiyo imetolewa Januari 27,2025,na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Erasto Siima wakati wa mahonjiano na vyombo mbalimbali vya habari wilayani humo mkoani Kagera.
Siima,amesema,zao la kahawa ni tegemeo la kukuza uchumi wa Mkoa wa Kagera na Wilaya ya Bukoba,ambapo kwa sasa umeibuka ugonjwa unaoshambulia mmea wa zao hilo.
” Hili jambo ikiendelea litashusha uchumi wetu, wataalam wa kilimo,wapo maeneo ya mashamba ya kahawa kuangalia namna ya kufanya utatuzi.Nimeagiza wataalam wa kilimo kuangalia hasa maeneo yaliyo na uharibifu ili kuweza kushughulikia changamoto hiyo,”.
Awali Ofisa Kilimo kutoka Halmashauri ya Bukoba,Babylus Mashauri,akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani,amesema Halmashauri hiyo imepata changamoto ya kisumbufu kinachoshambulia zao la Kahawa kinaitwa bungua mweusi wa Kahawa.
Mashauri,amesema mududu huyo anashambulia matawi ya mmea wa kahawa kwa kutoboa matundu madogo na kuingia ndani kisha anataga mayai na kuzaa.
Amesema bungua wa kiume anaweza kuishi siku 6 huku bungua wa kike anaishi siku 58 na ana uwezo wa kutaga mayai kati ya 20 hadi 50, kwa uzao mmoja, lakini baada ya kuanguliwa hao wadudu bungua wa kike anakaa siku ( 19 ) kisha anaondoka kwenda kutafuta makazi mengine.
Bungua huyo ukausha matawi yaliyoshambuliwa na kadri anavyoendelea kushambulia athari inaweza kuwa kubwa na kusababisha zao la kahawa kupoteza uzalishaji kwa kiwango kinachoanzia asilimia 20 hadi 50.
Hata hivyo amebainisha kuwa mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huo, ni pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wa kilimo kwa maana ya kuwatambua wadudu pamoja na madhara yake.
Huku hatua ya pili ni kampeni kwa ajili ya kumtokomeza mdudu huyo mwenye madhara kwa jamii inayojishughulisha na zao hilo kwa ajili ya kujiongezea kipato.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Murshid Ngeze ,amemuomba Mkuu wa Wilaya kuwasaidia katika kukabiliana na tatizo la ugonjwa huo unaotishia maisha ya wakulima wa kahawa.
Ngeze ,amewataka wataalam wa kilimo kutafuta suluhisho la haraka ili kudhibiti tatizo hilo kabla alijawa kubwa.
More Stories
Premium Active Tanzania yapunguza uhaba wa madawati Mlele
TARURA Kilindi kutumia bil.5.2 bajeti 2025/26
Madiwani Kilindi wapitisha bil.36.8 bajeti 2025/26