November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bunge laridhia mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Mambo ya Kale na ya makumbusho ya taifa.

Na Penina Malundo, timesmajira

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt Pindi Chana amelishukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia mapendekezo ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Mambo ya kale Sura 333 ya mwaka 1964 na marekebisho yake ya mwaka 1979 pamoja Sheria ya Makumbusho ya Taifa Sura 281 ya Mwaka 1980.

Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana amesema chimbuko la kufanya marekebisho hayo ni hitaji la kutaka kuboresha mazingira na usimamizi wa sekta hiyo ambayo majukumu yake ya Kisera na Kiutendaji yalikuwa bado yanatekelezwa katika ngazi ya Wizara kupitia Idara ya Mambo ya Kale.

“Marekebisho haya yanalenga kuimarisha mfumo mzima wa kitaasisi wa usimamiaji wa rasilimalikale nchini kwa maana ya kuwa na Idara inayosimamia Sekta nzima na kuwa na taasisi inayotekeleza majukumu ya kiutendaji”. Amesema Balozi Dkt.Chana.

Ameongeza kuwa msingi wa marekebisho ya Sheria hizo unalenga kuakisi muundo wa Wizara uliopitishwa mwezi Januari 2022 ambao umehamisha majukumu ya kiutendaji kutoka Idara ya Mambo ya Kale kwenda Makumbusho ya Taifa la Tanzania.

“Marekebisho haya yatasaidia kuhamisha majukumu yote ya kiutendaji kutoka Idara ya mambo ya Kale kwenda Shirika la Makumbusho ya Taifa la Tanzania kama vile kuingia katika eneo ili kukagua malikale, kuweka ulinzi wa malikale na kufanyia utafiti wa malikale katika eneo lenye malikale; utafutaji wa malikale; utoaji vibali na usimamizi wa watafiti wa malikale”. Amefafanua Balozi Dkt. Chana

Aidha marekebisho yamefanyika ili kurusu usajili wa Makumbusho zinazoanzishwa na wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za Umma, Asasi za kijamii na watu binafsi ili kuzitambua na kuzisimamia kwa kutoa miongozo na kuhamasisha utalii wa utamaduni.