lNa Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
HATIMAYE Serikali ineridhia ombi la wafanyakazi kwa kupeleka Bungeni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kazi wa Mwaka 2024 unaolenga kuleta ustawi katika sekta ya kazi nchini hususan kuongeza likizo kwa wazazi wanaojifungua watoto njiti,muswada ambao umepitishwa na Bunge.
Katika muswada huo Serikali imeridhia Likizo ya uzazi kuongezeka kwa wazazi wanaojifungua watoto njiti ambapo mama anayejifungua mtoto atakuwa na likizo ya Hadi wiki 36 na baba atakuwa na haki ya kupata likizo ya siku 14 Ili kuwapatia wazazi hao muda wa kulea na kumtunza mtoto lakini pia mama kupata muda wa kurejesha Afya yake.
Aidha Sheria nyingine zilizofanyiwa marekebisho ni Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini, Sura ya 366, Sheria ya Taasisi za Kazi, Sura ya 300 na Sheria ya Usimamizi wa Ajira za Wageni, Sura ya 436.
Muswada huo umewasilishwa Bungeni na Waziri wa Madini Anthony Mavunde kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete, ambapo anesema amesema likizo ya uzazi kwa mwajiriwa ambaye atajifungua mtoto njiti itajumuisha na muda uliobaki kufikia wiki 40 za ujauzito.
Aidha, amesema kifungu kipya cha 34A kinalenga kumwezesha mwajiri kumpatia mwajiriwa likizo bila malipo isiyozidi siku 30 ili kuweka mazingira mazuri yatakayomwezesha mwajiriwa kupata likizo bila malipo kutokana na majanga au dharura zinazoweza kujitokeza.
Pamoja na hayo, kifungu cha 14 kimebainisha aina ya mikataba ya muda maalum ili kuongeza wigo wa mazingira ambayo mtu anaweza kuajiriwa kwa mkataba wa kipindi maalum.
Katika kifungu cha 37, amesema kimeweka masharti yanayozuia mwajiri kutoanzisha au kuendelea na shauri la nidhamu dhidi ya mwajiriwa pale ambapo mgogoro huo upo mbele ya Tume au Mahakama ya Kazi ili kuzuia uingiliaji wa mchakato kushughulikia migogoro.
Vilevile, kifungu cha 71 kimeweka masharti ya utaratibu wa kuanza kutumika kwa mikataba ya hali bora inayoingiwa na wakuu wa taasisi za umma.
Mavunde amesema kifungu cha tisa cha Sheria ya Usimamizi wa Ajira za Wageni, Sura ya 436 kimeweka masharti ya kumtaka Raia wa kigeni mwenye kibali cha kazi daraja A anayekusudia kujihusisha na kampuni nyingine anayomiliki hisa kupata idhini ya Kamishna wa Kazi badala ya kibali kingine cha kazi.
Akisoma maoni ya Kamati Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Fatuma Toufiq, amepongeza serikali kwa kufanya marekebisho ya sheria hiyo na kukubaliana na maoni ya kamati ili kuleta ustawi wa wafanyakazi na watoto nchini.
More Stories
Wanachi wahimizwa kusajili biashara,majina ya kampuni BRELA
GreenFaith yatoa mapendekezo yake mkutano wa mission 300 kwa Wakuu wa nchi,Serikali za Afrika
Mwenyekiti UVCCM ataka wakandarasi kuwa na weledi ujenzi wa miradi