December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bunge laidhinisha Bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Na Mwandishi wetu, Dodoma

Bunge limepitisha makadirio na mapato ya mapato na matumizi ya Shilingi 35,445,041,000 ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa lengo la katika kuwahudumia Watanzania.

Wabunge wamefikia uamuzi huo Bungeni, Juni 6, 2023 mchana jijini Dodoma mara baada ya kujadili mpango wa Wizara hiyo uliowasilishwa na Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana.

Aidha, Balozi Dkt. Chana amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia Tanzania kushirikiana na Kenya na Uganda kuomba kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Mpira wa Miguu barani Afrika (AFCON 2027) ambayo ni mashindano mkubwa barani Afrika.

Kwa upande wake Naibu Waziri Mhe. Hamis Mwinjuma akifafanua hoja ya Mbunge wa Makete Festo Sanga kuhusu ujenzi wa viwanja vya michezo, amesema kuwa kampuni zinazotekeleza miradi mikubwa nchini zinatakiwa kutumia sehemu ya mapato yao kurudisha kwa jamii (CSR) ili kusaidia kutengeneza miundombinu ya michezo nchini kutoka katika sekta za fedha, nishati na madini na tayari Wizara imeanza kufanya mawasiliano na Wizara husika na mawasiliano yanaendelea vizuri hatua inayosaidia kufikia malengo ya Serikali.

Akichangia mjadala kwenye bajeti hiyo, Mbunge wa Bunda Mjini Mhe. Ester Bulaya amesema kuwa Wizara hiyo ina bajeti ndogo hivyo waongezewe hela, itatengeneza ajira mpya, ikipewa fedha za kutosha taifa litakuwa na furaha kwa kuwa Watanzania wanapenda michezo ili kupata viwanja bora na timu imara ambazo zitakuwa na ushindani katika uga wa kimataifa.