Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Zanzibar
BAADHI ya wananchi wa Jimbo la Bumbwini Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja wameeleza kuridhishwa na kasi ya maendeleo yaliyofanywa kwa kipindi cha miaka mitano,na mgombea kiti cha Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapindizi(CCM),Dkt.Hussein Ali Mwinyi, ikiwemo kuimarisha maendeleo katika nyanja za kiuchumi na kijamii.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mahojiano maalum,wameeleza kuwa Dkt.Mwinyi ametekeleza kwa ufanisi aahadi mbalimbali zilizotolewa katika kampeni zilizopita sambamba na miradi mingine ya ziada kulingana na mahitaji ya wananchi wa jimbo hilo.

Akizungumza mkaazi wa Shehia ya Bumbwini Kidanzini Khamis Abdalla Haji,amesema katika kipindi cha miaka mitano ya Dkt.Mwinyi amefanya mambo mengi ikiwemo ujenzi ya hospitali ya kisasa ya Wilaya ya Pangatupu yenye vifaa tiba vya kisasa,wahudumu wa afya na madaktari wanaotoa huduma bora kwa wananchi wa jimbo hilo na maeneo jirani.
“Zamani ukiwa na mgonjwa ukipata rufaa lazima umpeleke mgonjwa hospitali ya Mnazi Mmoja ambapo kwa mwananchi wa kawaida ilikuwa ni changamoto kwa umbali lakini kwa sasa mgonjwa akiumwa unaweza kumpeleka hata kwa bodaboda akapatiwa matibabu kwa muda na kumrejesha nyumbani,”.
Pia kumejengwa nyumba za madaktari wanaoishi pale ili watoe huduma kwa wananchi saa 24,hali ambayo ni faraja kwa wananchi wa jimbo hilo na maeneo mengine jirani pamoja na kupata vipimo vyote vya maabara bila malipo.
Khamis,amesema kwa upande wa maendeleo ya miundombinu kuna ujenzi wa barabara kutoka Bumbwini kwenda Mahonda hadi Zingwezingwe Kazole mpaka Donge ili kurahisisha huduma ya usafiri kwa wananchi.
Katika maelezo yake Khamis,amesema serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa Bandari ya kisasa ya Mwanga Pwani kwa lengo la kutoa ajira kwa vijana na wananchi wa jimbo hilo na maeneo mengine ya Zanzibar na nje ya Zanzibar.
Naye Mwajuma Zununi Omar,amesema uongozi wa Dkt.Mwinyi,umeleta suluhu ya kumaliza changamoto za sekta ya elimu jimboni humo kwani zimejengwa shule mbalimbali za ghorofa.
Shule hizo ni.pamoja na ya Sekondari ya Balozi Seif Ali Idd na sekondari ya Makoba,zilizomaliza changamoto za wanafunzi kukaa wengi katika darasa moja hali iliyokuwa ikichangia kutofaulu katika mitihani mbalimbali ya kitaifa.
Pamoja na hayo amezungumzia namna wanawake wa jimbo hilo walivyonufaika na fursa za serikali ya awamu ya nane chini ya Uongozi wa Dk.Mwinyi,amesema kundi hilo linapata mikopo ya masharti nafuu inayowasaidia kuendesha shughuli za ujasiriamali na kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao ya kila siku.

“Wananchi wa Jimbo la Bumbwini hatuna cha kumlipa Dk.Mwinyi zaidi ya kumuombea maisha marefu na kumpigia kura ili apate ushindi katika uchaguzi huu ili aweze kuendelea kutekeleza maendeleo kwa manufaa ya yetu sote,”amesema Mwajuma.
Mwajuma,amesema wananchi wa jimbo hilo maisha yao yameimarika kwa kiwango kikubwa kutokana na uwepo wa miundombinu imara na rafiki inayowawezesha wananchi wa makundi mbalimbali kujiajiri wenyewe katika sekta za kilimo,uvuvi,biashara,ujasiriamali na ufugaji.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi