November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bumbuli watakiwa kumaliza miradi kwa wakati

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Bumbuli

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mwantumu Zodo ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli iliyopo wilayani Lushoto kuharakisha ujenzi wa miradi mikubwa ya wananchi na kuikamilisha kwa muda uliopangwa.

Zodo ameyasema hayo alipofika kukagua miradi ya shule za msingi Shashui na shule ya msingi mpya ya Mpalai pamoja na hospitali mpya ya Halmashauri ya Bumbuli.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mwantumu Zodo (kulia) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli Baraka Zikatimu (kushoto), mara baada ya kufika kukagua ujenzi wa hospitali mpya ya Halmashauri ya Bumbuli inayojengwa Kijiji cha Kwehangala

Zodo amesema serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari, huku zile za zamani zikiongezewa vyumba vya madarasa na ofisi za walimu, zahanati, vituo vya afya na hospitali hivyo miradi hiyo lazima ikamilike kwa wakati.

“Serikali imeleta fedha nyingi kwa miradi kama hii mfano shule ya msingi Mpalai ambayo ni shule mpya kabisa kupitia Mradi wa Boost imepewa kiasi cha milioni 446.5,shule ya msingi Shashui imepewa milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitano vipya vya madarasa hivyo mnatakiwa kukamilisha miradi hii kwa wakati ili iweze kuleta tija,”amesema Zodo.

Wanafunzi Shule ya Msingi Shashui wakiwa kwenye madarasa mapya na madawati mapya

Akisoma taarifa ya mradi wa shule ya msingi mpya ya Mpalai,Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Kwehangala Mary Kidavo amesema Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ilipokea fedha kupitia mradi wa Boost kiasi cha milioni 446.5 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo mpya inayojengwa katika Kijiji cha Mpalai.

Amesema mradi huo unatumia Force Account ulianza kutekelezwa Juni 20, 2023, na unatarajiwa kukamilika Septemba 30, 2023.

Sehemu ya vyumba vitano vipya vya madarasa Shule ya Msingi Shashui

“Baada ya mapokezi ya fedha, halmashauri ilipokea maelekezo ya matumizi ya fedha hizo kutoka TAMISEMI kuwa ni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya majengo saba ikiwa ni jengo la utawala milioni 77.7, nyumba ya walimu milioni 98, vyumba saba vya madarasa milioni 175, vyoo matundu sita kwa shule ya awali milioni 69.1, ujenzi wa vyoo matundu 10, ambapo 4 wavulana na 4 kwa wasichana huku matundu mawili ya walimu kiasi cha milioni n21 na ujenzi wa kichomea taka milioni 5.7,”amesema Kidavo.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Shashui iliyopo Kata ya Soni, Ibahati Sheiza amesema Halmashauri ya Bumbuli katika mwaka wa fedha 2022/2023 ilipokea kiasi cha milioni 100 kwa ajili ya vyumba vitano vya madarasa.

Mradi unatekelezwa kwa Force Account, ulianza utekelezaji Mei 20, mwaka huu, na umekamilika kwa asilimia 100.

Aidha amesema kiasi cha fedha kilichotumika ni zaidi ya milion milioni 85.9 huko kiasi kilichobaki kwenye akaunti ni zaidi ya milioni 14, ambayo ni malipo ya mwisho ya fundi na malipo ya madawati, milango, meza na viti ambavyo fundi anamalizia kazi yake.

Moja ya majengo ya hospitali mpya ya Halmashauri ya Bumbuli iliyopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga inayojengwa Kijiji cha Kwehangala, Kata ya Dule B yalipo makao makuu ya halmashauri hiyo

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli Baraka Zikatimu alimuahidi Zodo kuwa miradi yote ikiwemo hospitali mpya ya Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli itakamilika kwa wakati.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Diwani wa Kata ya Dule ‘B’ Ali Mkwavingwa amesema anaishukuru serikali kwa kupeleka miradi mikubwa kwenye kata yake ikiwemo shule ya msingi Mpalai, shule ya sekondari mpya na hospitali ya Halmashauri ya Bumbuli, ambapo pia kata hiyo ndiyo itakuwa Makao Makuu ya Halmashauri ya Bumbuli.

Moja ya vyumba vya madarasa Shule mpya ya Msingi Mpalai iliyopo Kata ya Dule B, Halmashauri ya Bumbuli, ambapo inajengwa kwa fedha za Mradi wa Boost
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mwantumu Zodo (katikati) akipanda mlima kwenda kukagua ujenzi wa Shule mpya ya Msingi Mpalai. Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bumbuli Hozza Mandia (wa pili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli Baraka Zikatimu (kulia), Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Lushoto Hamidah Kilua (wa pili kulia), na Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji UWT Mkoa wa Tanga Swahiba Mzee (kushoto)