Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Bumbuli
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli iliyopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Ameir Sheiza amesema watatekeleza miradi ya maendeleo kwa fedha za mapato ya ndani kwa kuangalia vipaumbele.
Ni baada ya baadhi ya madiwani kuhoji ni vipi halmashauri hiyo imeweza kukusanya fedha kupitia mapato ya ndani kwa zaidi ya asilimia 100 kwa mwaka wa fedha 2023/2024, lakini baadhi ya miradi imeshindwa kutekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani.
Wameyasema hayo Novemba 6, 2024 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani robo ya kwanza, wakati wanajadili taarifa ya Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango (FUM) ambayo iliwasilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Hozza Mandia kwa niaba ya Mwenyekiti, Sheiza.
“Tutatekeleza miradi ya maendeleo kwa mapato ya ndani kutokana na vipaumbele na namna bajeti itakavyoruhusu. Wote mnajua, halmashauri yetu ilikuwa inakusanya mapato ya ndani kwa mwaka chini ya asilimia 70 hadi 60, lakini mwaka 2023/2024 ni kweli tumekusanya asilimia 102 ya bajeti yetu, lakini bado tuna miradi mingi inayotakiwa kutekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani” alisema Sheiza.
Akichangia taarifa ya Kamati ya FUM, Diwani wa Kata ya Dule B Ali Mkwavingwa alisema moja ya sehemu ya miradi ambayo ilitakiwa itekelezwe kwa fedha za mapato ya ndani ni mfereji wa umwagiliaji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji mboga mboga Kijiji cha Wena, Kata ya Dule B.
“Mwenyekiti, kwenye bajeti ya 2023/2024 kupitia Own Source (Mapato ya Ndani), kuna miradi tuliipanga kuitekeleza kupitia mapato ya ndani. Moja ya miradi hiyo ni ule mradi wa ufukuaji wa mfereji wa wakulima Wena, na tuliupangia bajeti ya sh. milioni 12. Huku kwetu Bumbuli hakuna dili nyingine zaidi ya kilimo, na hasa kilimo cha umwagiliaji.
“Sasa naendelea kuuliza, pale Wena na sehemu nyingine ya halmashauri ambapo tulipanga fedha za mapato ya ndani zikatekeleze miradi hii, ni lini fedha hizi zitakwenda, hali ya kuwa tulishakusanya mapato ya ndani hadi asilimia 102, kwani naamini kwa kufanya hivyo tutakuwa tumewasaidia sana wananchi wetu, maana hawana kitu kingine cha kuwaingizia mapato zaidi ya shughuli za kilimo” alisema Mkwavingwa.
Naye Diwani wa Kata ya Mahezangu Rashid Sebarua alisema halmashauri hiyo ingeweza kupata fedha nyingi iwapo juhudi za ukusanyaji mapato zingeongezwa, kwani yeye akiwa mkulima wa mkonge, wakati mwingine analipia ushuru wa mkonge wilayani Korogwe badala ya Bumbuli sababu huwa hawaoni wakusanya ushuru huo kutoka Halmashauri ya Bumbuli wakiwa na mashine ya POS.
Sebarua alisema kwenye geti la ushuru la Msamaka na Mahezangulu yaliyopo kwenye kata yake, kila siku kuna zaidi ya Fuso ama Canter nane zinatoka na miwa huko, hivyo umakini unahitaji ili kuona ushuru unalipwa ili kuongeza mapato ya halmashauri.
Akijibu hoja hizo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli Magdalena Utoh alisema fedha zinazokusanywa kutokana na mkonge zinalipwa kwa kutumia Kumbukumbu ya Malipo (Control Number) badala ya kutumia Mashine ya Kielektroniki ya POS, na hiyo ni kutokana na mkonge, chai na kahawa, malipo yake ni ya fedha nyingi, hivyo hawawezi kuruhusu wanaokusanya ushuru kwa POS wakutane na fedha hizo, inaweza kuleta shida baadae.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli Baraka Zikatimu, aliwahi kusema kwenye moja ya vikao vya Baraza la Madiwani kuwa, halmashauri hiyo iliidhinishiwa na Baraza la Madiwani kukusanya sh. 1,122,613,000, lakini iliweza kukusanya sh. 1,149,000,000 sawa na asilimia 102. Ni katika mwaka wa fedha 2023/2024.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi