Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya amesema nguvu zake kwa sasa zimejikita katika kuhakikisha wananchi wa jimbo hilo wanapata maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza Mei 17, 2026 katika mkutano wa hadhara ulioongozwa na Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi mjini Bunda mkoani Mara, Bulaya amesema kipaumbele chake ni kuboresha huduma muhimu kwa wananchi ikiwemo maji safi na salama, miundombinu ya barabara, masoko, dampo la kisasa pamoja na stendi za mabasi.
Bulaya amesema katika bajeti ya maji ya mwaka 2026/27, jimbo la Bunda Mjini limetengewa Sh9.5 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji inayolenga kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.
“Kwa sasa tunataka kuhakikisha wananchi wa Bunda Mjini wanapata maendeleo yanayoonekana na kugusa maisha yao ya kila siku. Tumeelekeza nguvu katika miradi ya maji, barabara, masoko na huduma nyingine muhimu kwa maendeleo ya jimbo letu,” amesema Bulaya.
Aidha, amesema utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kufungua fursa za kiuchumi, kuongeza mazingira bora ya biashara na kuboresha ustawi wa wananchi wa Bunda Mjini.
Kwa upande wake, Kihongosi amempongeza Bulaya kwa juhudi zake za kusimamia maendeleo katika jimbo hilo, akisema utekelezaji wa miradi mbalimbali umeendelea kuimarisha huduma kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya eneo hilo.

More Stories
Wakazi kunduchi kunufaika huduma za Yas, Mixx
IFC, BII na Norfund zaipa NMB ufadhili wa Dola Mil. 180
Barabara zilizoathiriwa na mvua zipewe kipaumbele