December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bugando yashauri upimaji saratani mara kwa mara

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Kwa mujibu takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani (IARC) za 2018, zinaonyesha kuwa tatizo la saratani nchini Tanzania limekuwa likiongezeka siku hadi siku ambapo inakadiriwa kuwa katika kila watu100,000, watu 76 hugundulika kuwa na ugonjwa huo

Jamii imeshauriwa kuwa na utamaduni wa kupima na kuchunguza magonjwa yatokanayo na saratani mara kwa mara ili kuweza kutambua viashiria vya vya ugonjwa huo katika hatua za awali badala ya kusubiri saratani kufika hatua ya mbaya ambayo haiwezi kutibika.

Wito huo umetolewa Mkurugenzi wa huduma za Tiba wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Dkt. Bahati Wajanga,kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo,Novemba 8, 2022 ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya siku ya Mionzi Duniani.

Ambapo kwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando imeadhimishwa kwa kuendesha zoezi la uchunguzi na upimaji wa saratani ya ini,saratani ya matiti na saratani ya tezi dume kwa kutumia mawimbi ya sauti (Ultra sound) huku lengo kuu la zoezi hilo likiwa ni kujenga uelewa na mwamko wa kupima saratani ili kuwaokoa wananchi.

Dkt.Wajanga, ameeleza kuwa hospitali hiyo kwa kushirikiana na Idara ya Radiolojia imeandaa utaratibu wa kupima vipimo vya saratani ya ini na saratani ya matiti huku muitikio ni mkubwa na wananchi wanahamasika.

“Niwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi yanapotokea maadhimisho kama haya hasa wanaume kwani saratani ipo pande zote mbili na pia kujenga utamaduni wa kuchunguza magonjwa haya,”ameeleza Dkt.Wajanga.

Daktari Bingwa wa mionzi Dkt. Magreth Magambo ameeleza kuwa, kwa sasa wananchi wa Kanda ya Ziwa wanasumbuliwa na saratani.

Ambapo amezitaja dalili za saratani ya matiti kuwa ni pamoja na chuchu kutoa damu hivyo ni muhimu wanawake na wanaume kupima saratani ya matiti kwani wengi wao wanafika hospitali wakiwa katika hatua mbaya.

“Kati ya wagonjwa 100 kwa mwaka jana, 40 wameathirika lakini 10 kati yao wapo hatua mbaya tujenge mazoea ya kupima mara kwa mara walau mara moja kwa mwaka hasa kwa wenye umri wa kuanzia miaka 40,”ameeleza Dkt.Magambo.

Mkuu wa Idara na Daktari Bingwa wa magonjwa ya saratani wa Hospitali hiyo, Dkt. Nestory Masalu ameeleza kuwa kwa sasa Radiolojia inatumia mashine ya kisasa zaidi inayoitwa Mammografia kupima saratani ya matiti huku akiongeza kuwa Mwaka uliopita kati ya wagonjwa 240 wapya walifika wakiwa katika hatua ya tatu na ya nne na kutoa wito kwa jamii kufanya uchunguzi an vipimo mapema.

Ameongeza kuwa chanzo cha saratani ya mapafu husababishwa na moshi wa kuni pamoja na tumbaku huku akisisitiza suala la uchakataji wa tumbaku kuwa unaathiri mama na mtoto kwa kufua nguo zenye harufu ya tumbaku.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi waliofika kupata huduma ya vipimo wameushukuru uongozi wa Hospitali ya Bugando kupitia Idara ya Radiolojia wamesema kuwa, afya ndio utajiri mkubwa wa binadamu na ikitokea fursa kama hii wajitokeze huku wakiomba uongozi wa hospitali hiyo kuwa zoezi la uchunguzi bure liwe endelevu ili kuwasaidia wananchi.

Mkurugenzi wa huduma za Tiba wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Dkt. Bahati Wajanga(wa pili kulia) akiwa na wataalamu wa afya wa hospitali hiyo,Novemba 8, 2022 ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya siku ya Mionzi Duniani.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupima saratani katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ,Novemba 8, 2022 ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya siku ya Mionzi Duniani.