January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BRELA yawataka wafanyabiashara kujisajili

Penina Malundo, TimesMajira Online

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewataka wafanyabiashara nchini kuhakikisha wanasajili biashara zao na majina ya Kampuni iliwaweze kuzirasimisha rasmi biashara zao wanazoziendesha.

Akizungumza katika maonesho ya 45 ya Biashara ya kimataifa ya Sabasaba, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa BRELA, Roida Andusamile amesema, zoezi la usajili wa biashara na Makampuni wanaloliendesha gharama zake ni nafuu ambazo wafanyabiashara wanaweza kuzimudu.

Amesema, wananchi wasiogope kurasimisha biashara zao kwani ni rahisi na ina faida nyingi katika ufanyaji biashara ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa mikopo, zabuni mbalimbali ambazo mara nyingi upatikanaji wake ni lazima mfanyabiashara awe amesajiliwa na BRELA.

“Wananchi wengi hawana uelewa vizuri juu ya kujisajili kwa njia ya mtandao,ila sisi tumejipanga kutoa elimu zaidi ili kutoa uelewa juu ya kujisajili kwa njia ya mtandao na tumeanza kutoa mafunzo kwa Maafisa biashara kusaidia watu wanaopata changamoto kama hawa katika kusaidia kusajili majina ya biashara na Makampuni,”.

“Tumeshafanya mafunzo katika Kanda mbalimbali ikiwemo Kanda ya kati na Kanda ya nyanda za juu kusini,tutaendelea kwenda katika kanda nyingine,” amesema Roida.

Kila mwaka BRELA imekuwa ikishiriki maonesho ya Sabasaba ambapo mwaka huu, wamekuja na mtazamo mpya wa kuweka banda kubwa nje kwa lengo la kusogeza huduma kwa wateja wao.

Amesema, kutokana na usajili wa BRELA kuwa wa mtandao kuna baadhi ya wananchi wanapata changamoto ya kusajili kwa njia hiyo hivyo uwepo wao katika maonesho hayo ni njia pekee ya kuwafikia wanaopata changamoto kusajili majina ya biashara na kampuni.

“Tumepata watu wengi sana tangu maonesho yameanza tarehe 28 hadi Julai 4, 2021 tulisajili zaidi ya 100 na tunaimani hadi maonesho haya yamalizike tutakuwa tumesajili zaidi ya wafanyabiashara 500 na wanapata cheti hapa hapa baada kukamilisha matakwa ya Msingi ya usajili,”amesema

Amesema, BRELA ni wakala wa serikali iliyoanza kwa Sheria za wakala wa serikali namba 30 ya mwaka 1997 na kuanza kufanya kazi mwaka 1999 tangu ilipoanzishwa majukumu yanayofanya na wakala ni pamoja na kusajili majina ya biashara,makampuni,nembo za biashara,utoaji wa ataza,leseni za biashara kundi A ambazo zina mtazamo wa kitaifa na kimataifa pamoja na leseni ya viwanda .