Na Mwandishi Wetu
WAZALISHAJI, wafanyabiashara na wawekezaji wametakiwa kufika kwenye mabanda ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) yaliyopo kwenye Viwanja vya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba kupata huduma mbalimbali zinazotolewa BRELA.
Wito huo ulitolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa BRELA, Roida Andusamile, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho hayo yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Ametaja miongoni mwa huduma zinazotolewa na BRELA kwenye maonesho hayo kuwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wadau ili waweze kujua wanafanya nini.
Amesema BRELA ni kama lango la biashara, ndiyo maana kila mwaka wamekuwa wakishiriki maonesho hayo kwa sababu wazalishaji, wafanyabiashara na wawekezaji wanatakiwa kupitia BRELA kabla ya kuanza biashara zao.
“Mtu yeyote anayeanza biashara anatakiwa kusajili jina la Biashara, kusajili kampuni, kusajili Alama ya Biashara na Huduma, kupata Leseni ya Biashara kundi “A” na kama anaanzisha kiwanda, kupata leseni ya viwanda,” amesema Andusmile.
Amesema BRELA ipo kwa ajili ya kusaidia wawekezaji na wafanyabishara wote hata wale waliopo nje wanaotaka kuwekeza Tanzania, kwani lango lao la kwanza ni BRELA.
Andusamile amewataka wadau hao kutumia fursa ya maonesho hayo kupata huduma zinazotolewa na BRELA kwa sababu kwaka huu wameshiriki tofauti kidogo na miaka ya nyuma.
Kwa mujibu wa Andusamile, mwaka huu wapo kwenye mabanda manne, ambapo banda la kwanza lipo nje ya Wizara ya Fedha na Mipango, ambalo limegawanyika sehemu mbili.
Amesema banda la kwanza linatoa huduma za BRELA kwa ujumla na banda la pili ni maalum kwa ajili ya masuala ya Miliki Ubunifu, kwani bado uelewa wake ni mdogo kwa Watanzania.
“Kwa hiyo kwa mwaka huu tumeona tutumie fursa hii kuwahamasisha wavumbuzi mbalimbali kusajili vumbuzi zao hasa kwa kuzingatia kwamba Tanzania tuna wataalam mbalimbali ambao wanavumbua vitu mbalimbali , lakini hawajui jinsi ya kulinda vumbuzi zao,” amesema Andusamile.
Amefafanua kwamba maonesho hayo ni fursa ya kuwahamasisha hao wavumbuzi, kusajili vumbuzi zao na hatimaye kuzilinda na kunufaika na vumbuzi hizo.
Aidha, amesema kuna banda lingine ndani ya Banda la Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ambapo wanatoa huduma za hapo kwa hapo kwa wadau.
“Lakini pia kwenye Banda la Kilimanjaro kuna afisa ambaye anatoa huduma za papo kwa hapo,” amesema Andusamile
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu