December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BREAKING NEWS: Wanafunzi wote Feza Boys wapata ufaulu wa juu

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

UONGOZI wa Shule ya Sekondari ya Feza Boys umesema shule hiyo imepata ufaulu wa juu katika matokeo kidato cha nne yaliyotangaza leo na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA).

Umesema wanafunzi wote 69 wa shule hiyo wamepata daraja la kwanza kati ya hao, wanafunzi 44 wamepata daraja la kwanza wakiwa na alama 7 na wamepata A masomo yote.

Akizungumza waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mwalimu wa Taluma wa Shule ya Feza Boys, Richard Mahina, amesema wanafunzi hao walipokua kidato cha pili walifanikiwa kuingia kwenye 10 bora katika mtihani wa Taifa mwaka 2020 ambapo wameendeleza ubora wao mpaka kufikia kidato cha nne.

“Hii ni kutokana na juhudi za Serikali ya awamu ya sita kupitia wizara ya elimu, kuweka mazingira mazuri na wezeshi hasa katika kutoa ushirikiano mashuleni ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora,” alisema.

“Ufaulu huu ni mzuri sana, ni fahari kubwa sana kwetu kama walimu,kama nchi yetu na jamii kwa ujumla kwasababu kikubwa unachotakiwa kwa mwalimu ni ufundishe na utoe matunda yaliyobora “

Pia amesema kutokana na NECTA kusitisha utaratibu wa kutangaza shule 10 bora na wanafunzi bora kwa matokeo ya kidato cha nne kwa sababu iliyoelezwa kwamba ni utaratibu usio na tija,shule hiyo imeupokea vizuri uamuzi huo na wapo pamoja na serikali.

“Ni kweli wanafunzi wanasoma katika mazingira tofauti, kikubwa ni kwamba wanafunzi wanasoma vizuri na bahati nzuri wanafunzi wetu wamefanya vizuri sana hivyo tupo pamoja na serikali uamuzi waliouchukua ni mzuri na sisi tunauunga mkono, ” alisema Mhina

Maina aliwapongeza wanafunzi wote wa kidato cha nne wote 69 ambao wamejitahidi kwa kuhakikisha wanakuwa na uthubutu katika masomo yao na kupeleka kutoa matokeo mazuri shuleni hapo.

Aidha Maina aliwashukuru wazazi wa wanafunzi hao na uongozi wa Feza kwa kuwapa ushirikiano hadi kupelekea kupata matokeo hayo huku akiwataka walimu wengine kuchukua mfano huo wa walimu wa mwaka jana.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule ya Feza Boys, Bussury Omary amesema walitarajia wanafunzi wao wangefanya vizuri kutokana na juhudi walizokuwa nazo katika kutaka kujifunza na kuwa na uelewa wa kutosha.

“Walituaminisha kwamba wanaweza na kweli wamefanikiwa, tunawashukuru wazazi, uongozi, walimu na wanafunzi wenyewe kwani wanafunzi hawa walichokifanya kinahitaji heshima ya juu, pia tunaishukuru serikali kwa kuondoa utaratibu wa kutaja shule na mwanafunzi bora kwani inaweza ikasaidia sana kuondoa wizi kwenye mitihani “

Omary alisema wanafunzi wote ambao wamefaulu wanawapatia zawadi kutokana na ufaulu wake lakini pia walimu ambao wamefanya wanafunzi hao kupata ufalu huo wanapewa pongezi zao.

Naye Mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya Feza Boys William Fedrick, aliwapongeza wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2022 kwa ufaulu wao mzuri, hali inayowapelekea wao kupata morari ya kusoma zaidi na hata kufanya vizuri zaidi katika mitihani yao ya mwaka huu.

Mwalimu wa Taluma wa Shule ya Feza Boys, Richard Mahina akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, baada ya shule yao kufanya vizuri katika mtihani wa Taifa kidato cha nne mwaka jana, kushoto ni mwalimu wa taaluma wa shule iyo,Richard Maina.
Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule ya Sekondali Fedha Boys’ akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, baada ya shule yao kufanya vizuri katika mtihani wa Taifa kidato cha nne mwaka jana,kushoto ni mwalimu wa taaluma wa shule iyo,Richard Maina.