Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
ALIYEKUWA Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameapishwa kuwa Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais Samia ameapishwa leo Ikulu jijini Dar es Salaam na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, kuchukua nafasi ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli aliyefariki juzi kwa tatizo la moyo katika Hospitali ya Mzena, iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mara baada ya kuapishwa, Rais Samia amekagua gwaride maalum lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kisha kupokea heshima ya kupigiwa mizinga 21.
Kuapishwa kwa Rais Samia kumeshuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Spika wa Bunge, Job Ndugai, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Katibu Kiongozi Dkt. Bashiru Ally.
Wengine ni Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete.
Amesema tofauti na viapo aliyowahi kula, kiapo cha leo ni cha juu katika nchi yetu akiwa na majozi tele na nchi ikiwa imetandwa na wingu zito la simanzi katika kipindi cha maombolezi.
Atatafuta kipindi kingine na kuongea na wananchi kuhusu matarajio na mustakabali wa nchi yetu. Amesema Rais Magufuli amemfundisha mengi, na alikuwa chachu ya mabadiliko.
Ameomba Watanzania kuwa na moyo wa subira na tuko imara kama taifa na wao viongozi wamejipanga kuendelea vizuri pale alipoachia. Amesema nchi ina hazina ya viongozi na nidhamu ya vyombo vya ulinzi na usalama. Amewahakikisha Watanzania kuwa hakuna jambo litakaloharibika.
Amesema wakati huu sio wakati wa kunyosheana vidole, tusahau yaliyopita, kushikamane tujenge Tanzania mpya.
More Stories
Rais Samia afanya uteuzi
Waliombaka, kulawiti binti wa Yombo, Dar jela maisha
BREAKING NEWS: Rais Dkt Samia afanya uteuzi na uhamisho wa viongozi mbalimbali usiku huu