November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BREAKING NEWS: Ngome ya uhalifu, Kijijini Mbezi Beach B yasambaratishwa rasmi(Picha )

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Mbezi Beach B

SERIKALI imetekeleza agizo la kubomoa makazi yasiyo halali katika eneo maarufu la Kijijini katika Kata ya Kawe, Mtaa wa Mbezi Beach B, Wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Wilaya baada ya siku 14 za kuwataka kuhama kwa hiari kupita muda mrefu, huku wakazi wa eneo hilo wakiendelea kukaidi agizo hilo.

Utekelezaji wa zoezi la ubomoaji ulianza mapema alfajiri leo bila kujali mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha ,huku likitekelezwa chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mtaa.

Wakati zoezi hilo likiendelea wakazi wa eneo hilo walisikika wakilia huku kukiwa kwenye hekaheka ya kujaribu kuokoa kinachowezekana bila kujali mvua kubwa iliyokuwa ikiendelea kunyesha leo alfajiri.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo ambaye jina lake halikupatikana, alisikika akisema; “Wenyewe wanaitaka barabara yao, bora tungefanya wenyewe maana tuliambiwa ila ndio ubishi umetufiikisha hapa

Tumeponzwa na hawa viongozi uchwara, waliotuambia hatutaondoka sababu wao ndo “wenye duka (CCM)” Mkuu wa Wilaya ni msimamizi tu wa duka, sasa leo msimamizi wa duka ndio kasimamia duka, sasa hapo nani zaidi?” aliongea kwa hasira mwanaume huyo.

TimesMajira online ilishuhudia zoezi la ubomoaji likiendelea huku kukiwa na  hekaheka za kuokoa vitu mbalimbali. Katika ubomoaji huo, walikuwepo wafanyakazi wa halmashauri wakisimamia na kukusanya mabati na mbao na kupakia katika moja ya lori lenye namba za usajili SM12739.

Nao askari wa Jeshi la Polisi waliokuwa wakisimamia zoezi hilo walipoulizwa kuhusu mwenendo wa zoezi hilo, walisema hapakuwa na upinzani wowote, wala kizuizi chochote na kwamba wakazi hao walitoa ushirikiano kwa kukusanya wenyewe vitu vyao.

“Hakuna vurugu yoyote, hakuna upinzani wala aliyekaidi, sisi kama polisi tuko hapa kuhakikisha kuna amani na zoezi hili linakamilika bila ubishi wala kikwazo chochote” alisema mmoja wa askari ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa madai kuwa sio msemaji wa jeshi hilo.