January 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BREAKING NEWS; Anna Mghwira afariki

ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira amefariki.

Mama Anna amefariki katika Hospitali ya Mount Meru leo majira ya saa 5 asubuhi alikuwa amelazwa akitibiwa kwa takribani wiki moja.

Marehemu aliwahi kugombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya chama cha upinzani cha ACT – Wazalendo. Alikuwa mwanamke pekee waliogombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2015.

Anna Mghwira alizaliwa Januari 23, mwaka 1959 mkoa wa Singida.

Alipata elimu ya Msingi katika shule ya Msingi ya Nyerere Road kati ya mwaka 1968 na 1974.

Aidha,alipata elimu ya sekondari katika shule za sekondari za Ufundi ya Ihanja baina ya mwaka 1975 hadi 1978, na shule ya Seminari ya Lutheran baina ya mwaka 1979 hadi 1981.

Huo ulikuwa ndio mwanzo wa safari yake ndefu ya kutafuta elimu. Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, Mghwira alijiunga na Chuo Kikuu cha Tumaini na kuhitimu na shahada ya Theolojia mnamo mwaka 1986.

Mwaka huohuo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na huko alihitimu na Shahada ya Sheria.

Mwaka 1999 Mghwira alijiunga na Chuo Kikuu cha Essex nchini Uingereza na mwaka 2000 alipokamilisha masomo yake na alitunukiwa Shahada ya Uzamili ya Sheria.