January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa

BREAKING: Maambukizi mapya 196, sasa Tanzania ina wagonjwa 480

Na WAJMW-Dodoma

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ametangaza ongezeko la wagonjwa wa Corona 196 nchini huku Tanzania Bara ikiwa na Wagonjwa 174 na Zanzibar wagonjwa 22 ambao walitolewa taarifa na Waziri wa Afya Wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid na kufanya idadi ya wagonjwa wa Corona nchini kufikia 480.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema hayo wakati akigawa magari 50 ya kubebea wagonjwa kwa wabunge wa majimbo mbalimbali tukio lililofanyika leo katika ofisi ya Waziri Mkuu iliyopo Mlimwa jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema jumla ya wagonjwa waliopona imeongezeka kutoka 48 hadi kufikia 197, huku Zanzibar waliopona wakiwa 36 na Tanzania bara 83. Pia Waziri Mkuu amesema kumekuwa na ongezeko la vifo vya watu sita (6) na kufanya kuwa na vifo vilivyotoka na Corona nchini kufikia 16.

Kati ya wenye maambukizi 297 waliobaki, 283 wanaendelea vizuri na tiba na kusubiri ufuatiliaji wa afya zao na wengine 14 wako chini ya uangalizi maalumu wa madaktari ambao wanahitaji oksjeni (Oxygen) ya kuwasaidia kupumua pamoja na wale wenye magonjwa mengine ambayo yamejitokeza kwenye wodi.

Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuwaondoa washukiwa waliokua karantini ambao walishatimiza siku 14 baada ya uchunguzi wa kiafya kuonekana hawana maambukizi na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Hadi kufikia jana tarehe 28 Aprili, watu 644 wameruhusiwa kutoka karantini katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Zanzibar, Kilimanjaro, Mwanza, kagera, Songwe, Kigoma na Dodoma.

Hata hivyo Waziri Mkuu amekemea tabia ya upotoshaji na utoaji wa takwimu ambazo sio rasmi na kuzua taharuki kwa jamii kwamba kila kifo kimetokana na Corona kuwa sio sahihi na kusisitiza kuwa kuna magonjwa mengine ambayo yanaua pia.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zote zinazotolewa na wataalamu wa afya huku Serikali ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuweza kupambana na vita hii ya ugonjwa wa Corona.

Katika makabidhiano hayo ya magari, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa magari 50 nchiniyenye Tsh. Bilioni 6 ili yaweze kuwezesha rufaa za akinamama Wajawazito na kuepusha vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na kukabiliana na magonjwa ya milipuko kama Corona.

Magari 18 yamepekwa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, magari 32 yatatumika kwa ajili ya vituo vya afya na Hospitali za Wilaya.

Aidha, Waziri Ummy amemshukuru Waziri Mkuu kwa kutoa ushirikiano mkubwa unaoutoa kwa Wizara ya Afya kwa kuwezesha mambo mbalimbali lengo likiwa ni kufikisha huduma bora za afya kwa wananchi wote.