Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa ACT – Wazalendo ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, leo Jumatano, Machi 06 2024, amejumuika pamoja na Viongozi, Wanachama, Wafuasi, Wapenzi wa Chama hicho na Wananchi wengine, katika Mkutano Maalum wa Hadhara, hapo katika Viwanja vya Las Vegas Mabibo, jijini Dar es Salaam.
Akihutubia katika Mkutano huo, Othman, kama ilivyokuwa kwa viongozi wengine wapya ambao wamechaguliwa, ameshukuru namna ambavyo zoezi la Uchaguzi lilivyokwenda kwa uadilifu ndani ya Chama hicho, sambamba na imani ambayo Wanachama wameidhihirisha kwa Viongozi Wapya, akiwemo yeye binafsi.
‘Walinipa imani, nami nikaahidi pamoja na wenzangu kuwapa imani”, amesema Mheshimiwa Othman huku akiahidi kutekeleza Dhana ya Manufaa kwa Watanzania wote, katika mnasaba wa Fursa na Matumizi ya Rasilimali muhimu ziliopo Nchini.
Amefahamisha kwamba kwa kushirikiana na Viongozi wote wa Chama hicho, hasa wale ambao wamechaguliwa sasa, watahakikisha dhamira hiyo inatekelezwa vyema na kwa mafanikio makubwa.
Naye, Kiongozi Mpya wa Chama, wa ACT-Wazalendo Doroth Semu ameshukuru na kuwapongeza wanachama na viongozi wote kwa kusimamia na kutekeleza kwa umakini kile alichobainisha kwamba “ni demokrasia ya kweli” kupitia mchakato wote wa uchaguzi wao wa ndani, ambao pia amesema “umekuwa wa haki na huru”.
“Sasa tunarudi katika maeneo yetu ya Kazi kuhakikisha tunakwenda kukabiliana na changamoto za wananchi kama tunavyosema “Taifa la Wote, Maslahi ya Wote; twendeni, wala tusiyafumbie macho matatizo ya wananchi”, amesema Kiongozi huyo.
Mkutano huo ambao umekuja kufuatia kwisha kwa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Uchaguzi wa Chama hicho uliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, pia Jijini Dar es Salaam, umelenga kutoa Matokeo mbele ya Wananchi na Wanachama, na kuwaleta hadharani baada ya kuwachagua Viongozi wa Ngazi mbali mbali, wakiwemo Mwenyekiti wao wa Taifa na Makamo Mwenyekiti, kwa Pande zote, Tanzania Bara na Zanzibar.
Viongozi mbali mbali wa Siasa, Dini, Jamii, Wanadiplomasia, na Watu Mashuhuri kutoka ndani na Nje ya Nchi, wamehudhuria katika Mkutano huo wa Hadhara ambao ni wa Kwanza, tangu kuja kwa Safu Mpya ya Uongozi wa Chama hicho, baada ya kwisha kwa muda wa Viongozi waliopita, pamoja na kukamilika kwa Mchakato wa Uchaguzi wa Ndani.
Aidha, kulitangulia Matembezi ya Wanachama wakiongozwa na Safu yote ya Viongozi Wakuu, kutokea Mlimani City, kupitia Barabara za Sam Nujoma na Morogoro, hadi vilipo Viwanja vya Las Vegas.
Waliohudhuria hapo ni pamoja na Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib, sambamba na Makamu Mwenyekiti Wapya wa ACT- Wazalendo wa Tanzania Bara, na pia Zanzibar, Is-haka Rashid Mchinjita, na Imail Jussa Ladhu; wakiwepo pia Mwenyekiti Mstaafu, Mhe. Juma Duni Haji, na Kiongozi wa Chama aliyemaliza muda wake, Zitto Zuberi Kabwe.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango