January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Boti za Samia kwa wavuvi zachochea ajira kupitia raslimali za ziwani, bahari

Na Abdallah Aduel, TimesmajiraOnline

SERIKALI ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuonesha kuwajali wananchi kupitia shughuli zao mbalimbali wanazofanya ili waweze kujiingizia kipato cha uhakika.

Miongoni mwa wananchi hao ni wale wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi ili waweze kunufaika na raslimali za bahari.

Kwa vitendo, Rais Samia amedhahirisha dhamira yake ya kuboresha maisha ya wavuvi kwa kutoa pesa nyingi kwa ajili ya kuiwezesha sekta ya uvuvi iweze kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi.

Lengo la hatua hiyo i kuhakikisha rasilimali zilizopo nchini zikiwemo za uvuvi zinazidi kunufaisha Taifa na Watanzania kwa ujumla.

Rais Samia amedhihirisha hilo pale alipogawa boti za kisasa 160 kwa wavuvi, ikiwa ni mradi wenye zilizogharibu sh. bilioni 11.5 kwa wavuvi wakiwemo wakulima wa mwani katika Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu, vyama vya ushirika vya wavuvi, vikundi na kampuni za uvuvi ili kuwawezesha kuvua kisasa, kwa uhakika na usalama, hivyo kukuza kipato chao.

Kiongozi huyo amekabidhi boti hizo mwaka huu Wilaya ya Kilwa, eneo la Kilwa Masoko wakati akiweka jiwe la msingi katika Bandari ya Uvuvi.

Akizungumza wakati akikabidhi boti hizo, Rais Samia alisema; “Boti hizi 160 zimetolea kwa mkopo wa masharti nafuu na unalenga kutoa ajira na kuongeza kipato cha jamii. Boti ndogo zitatumiwa na akina mama kulima mwani na kubeba mizigo, na zile kubwa zinakwenda kwenye kina cha maji marefu.”

Aidha, Rais Samia aliweka wazi kwamba Serikali haitarajii boti hizo kuleta ugomvi katika vikundi vya wakulima na wavuvi, bali zitumike kuimarisha uchumi wao.

Pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bandari ya Uvuvi ya Kilwa, Rais Samia pia aligawa boti 34 kati ya boti 160 ambazo zinatolewa nchi nzima.

“‘Serikali imejipanga kuhakikisha mazingira ya wavuvi na wakuzaji viumbe maji yanaimarika ndio maana leo nimegawa boti za kisasa zikiwa na kifaa cha kuonyesha upatikanaji wa samaki na uhifadhi wa samaki,’ amesema Rais Samia.

Boti hizi kwa ukanda wa bahari ya Hindi zipo 92 zikihusisha wavuvi na wakulima wa mwani.

Wakulima wa mwani wanapongeza hatua ya Rais Samia kuwapatia boti hizi, hasa kwa kuzingatia kwamba zimetolewa katika kipindi ambacho soko la mwani na bei yake ni nzuri.

“Tumepata boti hizo wakati muafaka, kwani baada ya kulilia soko kwa miaka 17, leo hii wakulima wa zao hili tumepata wanunuzi watatu wa bidhaa hizo, ambapo bei ya zao hili imepanda kutoka sh. 500 kwa Mwani mdogo hadi 1,000 na kutoka 1,000 kwa mwani mkubwa hadi kufikia 2000,” anasema Mkulima wa Mwani, Mwajabu Said.

Mwani ina uwezo wa kutengeneza bidhaa mbalimbali, zikiwemo sabuni, mafuta, visheti, juice, soda mapambo dawa pia chakula.

Naye Mkulima wa zao la mwani kutoka katika kijiji cha Mnazi kata ya Nalingu, Tukae Magongo, anampongeza Rais Samia kwa kuwapatia boti hizo, akisema zinaenda kuboresha shughuli zao.

Anasema wamekuwa kifungoni kwa miaka 17, ambapo mnunuzi alikuwa mmoja na alikuwa anapanga bei yake.

“Biashara ilianzia sh. 500 mpaka 1000-1300 na sasa sh. 2,000 hii inatunufaisha kwa kuwa hata ukiwa na kidogo unauza unapata pesa hali ya soko sio mbaya.

Tunao wanunuzi watatu sio sawa na mmoja aliyekuwa akinunua hapo awali, kwa hiyo boti hizo zitawezesha kuinua uwezo watu kiuchumi” alisema.

Naye Shakifu Kambwili Mkazi wa Kijiji cha Mnazi alisema anashawishika kuanza kulima zao hilo, kwa kuwa sasa hivi wana boti za kuwafanya wafikia raslimali hizo.

“Kwa sasa anaona hata mkulima akiwa na kilo mbili anapima na kupata pesa sio kumsubiri bosi aje,” anasema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mnazi, Faume Mchinji alisema kupanda kwa bei ya mwani ni msaada mkubwa kwa wakulima wa zao hilo, ambapo sasa watapata pesa na kununua vifaa vinavyofaa vinvyotumika kwenye zao hilo.

Naye Mustapha Kwiyunga, Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la Mtwara Society Against Poverty (Msoapo) anasema mpaka sasa vipo vikundi 30 vinavyozalisha zao la mwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, hivyo boti hizo zitakuwa msaada kwao.

“Awali tuliuza mwani mdogo 500 na mwani mkubwa 1,000 na mnunuzi alikuwa mmoja tulijitahidi kutangaza ambapo sasa tumepata wateja watatu, mama (Rais Samia) tupatia boti uzalishaji utaongezeka.” alisema.

Mnufaika wa mradi huo, Shukrani Shamte ambaye ni mkulima wa mwani ameipongeza Serikali kwa jitihada hizo za Serikali.

“Tunaikushuru Serikali kwa kutupatia mkopo wa boti ya malipo nafuu, boti hizi zitatusaidia kwenye shughuli za kulima mwani kwenye kina cha maji mengi na kubeba mwani kutoka kwenye maji mengi kuja Pwani.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema kuwa kati ya boti hizo zipo ndogo na zenye ukubwa wa mita 14 na uwezo wa kuhifadhi samaki hadi tani moja na nusu.

“Tunakushuru Rais kwa kutupa fedha sh. bilioni 11.5 zitakazowasaidia wavuvi na kazi imeanza.

Akizungumza wakati wa kukabidhi boti za 14 za uvuvi zilizotolewa na Rais, Samia , zenye thamani ya sh. Bilioni 1.2 kwa ajili ya kuwapa wavuvi mkoani Tanga ili wazitumie kuboresha shughuli zao, Waziri Ulega alisema;

“Rais Samia amedhamiria kuboresha maisha ya wavuvi na ndio maana anatoa pesa nyingi kwa ajili ya kuziwezesha sekta za uzalishaji ikiwemo sekta ya uvuvi ziweze kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi ili kuhakikisha rasilimali zilizopo nchini zikiwemo za uvuvi zinazidi kunufaisha Taifa na Watanzania kwa ujumla.”

Ulega alisema mpango huo unatekelezwa kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ambapo katika awamu ya kwanza jumla ya boti 160 zenye thamani ya sh. Bilioni 11.5 zitatolewa kwa wanufaika nchi nzima, huku zikitarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja kwa takribani watu 4,296 wakiwemo wavuvi mmoja mmoja, vikundi na vyama vya ushirika.

Ulega amekemea vitendo vya uvuvi haramu vinavyoendelea, huku akisisitiza kuwa boti hizo ni mahsusi kwa ajili ya uvuvi endelevu tu na si vinginevyo.

Anasema Serikali haitosita kuchukua hatua za kisheria ikigundua wavuvi wanajihusisha na uvuvi haramu au usafirishaji wa mazao haramu ya uvuvi.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Agnes Meena alisema boti hizo za kisasa zimetokana na mkopo nafuu usiokuwa na riba kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) ambao wanashirikiana na Serikali kuhakikisha wanakuza pato la wavuvi.

Rais Samia Suluhu Hassan, akiangalia boti mojawapo kati ya 160 alizonunulia wavuvi ili kuwawezesha kunufakaika na raslimali za bahari na ziwani.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba amemshukuru Rais, Dkt Samia kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuliongoza Taifa na kuliletea maendeleo ikiwemo boti hizo 14 zilizotolewa kwa mkoa wa Tanga, ambazo zitasaidia kusukuma mbele maendeleo ya wavuvi.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe, akizungumza Septemba 25, 2023 wakati wa uzindua na kukabidhi boti nne za doria zenye thamani ya 200M zilizotolewa msaada na taasisi ya The Nature Conservancy (TNC) kwa BMU’s tisa zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa, alimshukuru Rais Samia, kwa kuendelea kuwajali wa Wavuvi kote nchini.

Aasema katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa Rais ametoa jumla ya Boti 15 kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wavuvi kwa mkopo wa usiokuwa na riba.

Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Peter Lijualikali alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali wananchi wa Wilaya ya Nkasi kwa kutoa Boti 15 kwa ajili ya kuwakopesha Vikundi vya Wavuvi Wilayani Nkasi kwa mkopo usiokuwa na riba.