January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Boti za Rais Samia zabadilisha maisha wavuvi mkoani Mwanza

*Kipato chao chafikia milioni 12/- kwa mwezi

Na Judith Ferdinand,Timesmajiraonline, Mwanza

JANUARI 30, mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan, aligawa boti kwa wavuvi wa Ziwa Victoria mkoani Mwanza.

Rais Samia aligawa boti hizo kwa wavuvi kwa lengo la kutoa ajira na kukuza uchumi wa bluu kwa wavuvi na kuwaongezea tija kwenye shughuli zao.

Aligawa boti kisasa 55 kwa wavuvi wa Kanda ya Ziwa katika hafla iliofanyika jijini Mwanza. Tangu wavuvi wakabidhiwe boto hizo, wanasema kipato chao kimeongezeka kwa kutoka kuvua samaki wa kilo 20 hadi kilo 300 kwa wiki.

Kutokana na mafanikio hayo, wavuvi hao wanampongeza Rais Samia Suluhu Haasan ambapo wameihakikishia Serikali kuwa watarejesha mkopo wa boti hizo bila wasiwasi.

Wanataja siri ya mafanikio hayo ni boti hizo za kisasa ambazo wamekabidhiwa na Rais Samia kuwa na kifaa kinachoitwa fish finder’ ambacho kinasaidia kuonesha samaki waliopo.

Lakini kifaa hizo kinaelekeza mahali wanapotoka, wanakokwenda na walipo hali inayoelezwa kuwa ni rahisi hata kupata msaada endapo itatokea changamoto wakiwa kazini.

Wakizungumza na waandishi wa habari waliowatembelea wavuvi hao Juni 21,2024 baadhi ya wanufaika wa boti hizo katika mwalo wa Mswahili uliopo wilayani Nyamagana jijini Mwanza, wanampongeza Rais Samia kwa kuwapatia boti hizo, kwani zimebadilisha maisha yao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kikundi cha Tunza Mazingira Mkuyuni wilayani Nyamagana, Charles Lulinga, anasema kuwa
tangu wameanza kufanya kazi ya uvuvi kupitia boti hizo, wameweza kutunza akiba ya zaidi ya milioni tatu kwenye akaunti ya kikundi chao.

Wavuvi wa Mwalo wa Mswahili wakiwa ndani ya moja ya boti ya kisasa ya uvuvi iliyotolewa na Rais Samia, wakirejea mwaloni wakitoka kuvua ndani ya Ziwa Victoria.(Picha na Judith Ferdinand).

Anasema kuwa awali wavuvi walikuwa awathaminiki, kwani waliambiwa ni watu wasiokopesheka, hawadhaminiki na ni watu wa kuhamahama na wasiyo na elimu, lakini Rais Samia amewaheshimisha kwa kuwapa mkopo wa zana za uvuvi bila dhamana yoyote.

“Awamu hii imemtambua mvuvi na kumkopesha boti hizi ambazo zimetusaidia awali tulikuwa tunatumia boti za kawaida za mbao na baada ya Rais Samia kutuwezesha kupata vitendea kazi, ambavyo ni vya kisasa vimesaidia wafanyekazi kwa ubora na usalama zaidi na kikundi chao kinasonga mbele.”

Anasema wakati wa upepo walikuwa wanashindwa kwenda kuvua samaki, ibidi kuegesha pembeni boti zao, lakini uzuri wa boti hizi za kisasa zinafanyakazi.

Mwenyekiti wa BMU Mkuyuni, Robert Charles anasema kuwa wamepata faida nyingi kupitia boti hizo ikiwemo watu kupata ajira, hivyo ameiomba Serikali kuendelea kutoa boti hizo kwa wavuvi wa Kanda ya Ziwa, kwani zimeleta chachu ya kufanya kazi kwa kufika maeneo ya mbali zaidi .

Anasema mazao ya samaki yanapatikana kiurahisi tofauti na awali walikuwa wanatumia boti za kawaida ambazo haziwezi kufika mbali.

“Kanda ya Ziwa wavuvi tuwezeshwe zaidi zana hizo za uvuvi za kisasa, kwani nchini hapa kanda hii inategemewa katika pato la taifa na Ziwa Victoria ndilo ziwa Kuu linalosaidia katika masuala ya uvuvi katika mwalo huu wa Mswahili tuna vikundi vinne ambavyo vimewezeshwa na tunaendesha maisha yetu,” anasema.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Wavuvi Chembaya kilichopo Halmashauri ya Buchosha, Robert Lwanga, anasema kupitia boti hizo wameondokana na changamoto nyingi ambazo walikuwa wanazipata katika shughuli za uvuvi.

“Tumepunguza idadi kubwa ya ajali za kwenye maji,vifo vya wavuvi vilikuwa vinasababishwa na vyombo hafifu, lakini kwa sasa hivi watu wanaenda wakiwa katika usalama wa kutosha, boti zinahimili upepo, kwenye chama chetu pato limeongezeka kutoka kilo 20 mpaka 300 kwa siku saba.

Anasema kilo moja ya samaki wanauza sh. 10,000 hivyo kwa kilo hizo 300 ni sawa na sh. milioni 3 kwa wiki.

“Tunataweza kurejesha mkopo huo wa boti bila wasiwasi, kwani kwa mwezi tunatakiwa kurejesha milioni 1,”anasema. Anasema kwa sasa kipato chao kwa mwezi sh. milioni 12.

Mwanachama wa Ushirika wa Bukasiga Wilaya ya Ukerewe, Tecla Bwire, anasema; “Sisi ni wanufaika wa boti ya dagaa hivyo naomba Wizara itusaidie tuweze kupata hata boti tano, kwani samaki wana tabia ya kusambaa hivyo boti moja ikikosa nyingine inapata,” anasema.

Aidha Msiriakale Juma kutoka Chama cha Chembaya FICOS Buchosha, anasema boti hizo zina kifaa kinachoitwa ‘fish finder’ ambacho kina programu mbalimbali na matumizi yake ni kama simu janja ambacho kinawaleza zilipo .

“Ukienda sehemu ya umbali unakitoa kwenye ‘fish finder’ kinakupeleka kwenye ‘GPS’ kinakuelekeza kuwa sasa umetoka hapa unakwenda sehemu fulani kuvua na siku ukiwa unataka kurudi kinakuelekeza ulipotoka na ambaye hafahamu namna ya kukitumia ni vyema aende kwa wataalamu ili wamsaidie”.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt.Edwin Mhede,alieleza kuwa Serikali haitarudi nyuma katika kuboresha sekta hiyo ya uvuvi.

Anasema Serikali ameisha toa maelekezo kwa taasisi zinazohusika za kisekta kuhakikisha changamoto zilizo nje ya uwezo wa wavuvi na zinazohitaji utaalamu zinashughulikiwa.