October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BOT yasisitiza matumizi ya shilingi ya Tanzania

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

BENKI Kuu ya Tanzania (BOT)imeendelea  kusisitiza watoa huduma mbalimbali nchini kuacha kufanya malipo ya ndani ya nchi  kwa kutumia fedha za kigeni
ambapo imesema kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Hayo yalisemwa jijiji hapa leo,Oktoba 3,2024 na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania,Emmanuel Tutuba wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya Kamati ya ya sera ya fedha (MPC)  ambapo alisema Bodi ya wakurugenzi wa Benki kuu Tanzania iliyokutana Oktoba 2,2024 imeamua  Riba ya Benki Kuu (CBR) kuendelea kuwa asilimia 6
kwa robo mwaka itakayoishia Disemba 2024.

Ambapo amesema Uamuzi huo ulitokana na matarajio ya mfumuko wa bei kuendelea kuwa chini ya lengo la nchi la asilimia 5.

Tutuba ameendelea  kutoa rai watanzania wote kutumia shilingi za Tanzania kufanya malipo na huduma za bidhaa ndani ya nchi na kwenye sheria nakutamka kwamba mtu atakayefanya malipo kwa kutumia fedha za kigeni ,anapofanya malipo ya ndani ya nchi kwa kutumia fedha za kigeni atakuwa ametenda kosa.

Amesema matakwa ya kisheria ambayo wameendelea kusisitiza hususani kwa kufanya malipo ya ndani kwa kutumia shilingi ya Tanzania nayo yanaendelea kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni hapa nchini na kuongeza ufanisi wa sera ya fedha.

“Niendelee kutoa wito wa kuendelea kuzingatia sheria kama mnavyokumbuka wakati wa bajeti Waziri wa fedha wakati anasoma bajeti na wakati wa kupitisha sheria ya fedha mwaka huu,Serikali na Bunge waliliridhia kwamba tuendelee kusimamia sheria ambapo kifungu cha 26 cha sheria ya Benki kuu kinatamka kwamba benki kuu itachapisha fedha itakayoitwa shilingi ya Tanzania fedha hiyo ndiyo itakayokuwa fedha pekee hali kwa malipo yote ya ndani ya nchi.

“Kwahiyo niendelee kuomba Benki na watanzania wote kwa ujumla unaponunua bidhaa ndani ya nchi tutumie shilingi ya Tanzania kwasababu kufanya hivyo ndiyo tunaendelea kusapoti sera ya fedha,”amesema.

Tutuba ameeleza kuwa mtu anapofanya malipo ya bidhaa na huduma kwa kutumia shughuli za kitanzania lakini akatumia fedha za kigeni maana yake anafanya kosa ambalo kisheria na anastahili kupewa adhabu .

“Kwahiyo niendelee kuomba wale ambao wanapangisha nyumba ,wanatoa huduma mbalimbali za ada,wanafanya malipo wanatoa risiti na wengine wanashawishi na kutoa ankra(invoice) kwa kutumia fedha za kigeni kwa shughuli ambazo zipo ndani ya nchi wamefanya kosa ni waase waache kufanya hivyo,”amesema.

Hata hivyo amesema kuwa fedha za kigeni ziendelee kutumika tu pale ambapo mtu anafanya miamala inayovuka mipaka ni miamala kwenda nchi za nje hapo utakuwa umefanya biashara ya kimataifa na hapo ndipo unaporuhusiwa kutumia fedha za kigeni .

Aidha amesema benki kuu itaendelea kuimarisha akiba ya fedha za kigeni kupitia mpango wa ununuzi wa dhahabu katika soko la ndani kwa kutumia shilingi ya Tanzania .

Wakati huo huo,Tutuba ameeleza kuwa
Upatikanaji wa fedha za kigeni unatarajiwa kuendelea kuimarika, kutokana na ongezeko la bei ya dhahabu kwenye soko la dunia, shughuli za utalii na mauzo ya
bidhaa asilia kama korosho, tumbaku, kahawa na pamba.

“Mauzo ya mazao ya chakula
hususan mahindi na mchele kwenda nchi jirani, pia yanatarajiwa kuongeza mapato ya fedha za kigeni.

Hata hivyo amesema kuwa kupungua kwa uagizaji wa mbolea na kupungua kwa bei za bidhaa za mafuta ya nishati kunatarajiwa kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni.

Vilevile,amesema matakwa ya kisheria kuhusu kunukuu na kufanya malipo ya ndani kwa shilingi ya Tanzania yanatarajiwa kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni nchini na kuongeza ufanisi wa sera ya fedha.

Aidha,amesema Benki Kuu itaendelelea kuimarisha akiba ya fedha za kigeni.

Pamoja na hayo alitumia fursa hiyo kuwashukuru  wote wanaoendelea kuuza dhahabu zao benki kuu tangu kuanza kununua dhahabu hizo Oktoba Mosi,2024.