Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
BODI ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB),imeeleza kuwa katika uchunguzi wa awali wa kimaabara wamebaini uwepo wa kiwango kikubwa cha mafuta na kukosekana kwa hewa ya okisijeni kwenye maji.
Uchunguzi huo umefanyika baada ya LVBWB Machi 8,2022 kupokea taarifa ya uwepo wa uchafuzi wa maji uliosababisha maji kuwa meusi na kufa kwa samaki katika mto Mara kwenye eneo la Kirumi Darajani.
Ambapo vijiji vilivyoathirika na uchafuzi huo ni pamoja na Kirumi,Kwibuse,Marasibora,Ketasakwa na Ryamisanga.
Hayo yamezungumzwa na Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria Renatus Shinhu,wakati akitoa taarifa ya awali kwa umma katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za bodi hiyo, mkoani Mwanza.
Shinhu amesema Machi 8, mwaka huu bodi ilifika eneo la tukio na kuchukua sampuli za maji kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara ili kufahamu hali ya ubora wa maji.
Amesema,baada ya uchunguzi wa kimaabara ambao umeonesha mambo mawili ikiwemo kuwepo kwa kiwango kikubwa cha mafuta kuliko kiwango kinachokubalika kwa mujibu wa viwango vya ubora wa maji Tanzania ( TZs 2068:2017).
Pamoja na kukosekana kwa hewa ya okisijeni kwenye maji kuliko kiwango kinachokubalika kwa mujibu wa viwango vya ubora wa maji Tanzania.
“Kiwango kikubwa cha mafuta kwenye maji ndicho kilichosababisha kuisha kwa hewa ya okisijeni kwenye maji na kuathiri viumbe hai ikiwa ni pamoja na samaki,” na kuongeza kuwa
“Kuhusu rangi ya maji uchunguzi wa kimaabara unaendelea ili kubaini kilichosababisha maji haya kuwa meusi,” amesema Shinhu.
Pia ameeleza kuwa,kwa mujibu wa majibu ya maabara ya Machi 11 mwaka huu,kiwango cha okisijeni kwenye maji kinaongezeka na kiwango cha mafuta kinapungua.
Aidha amesema,wanaendelea kufuatilia kwa ukaribu ili kufahamu chanzo cha maji kuwa meusi na chanzo cha mafuta hayo ni nini,hivyo wataendelea kutoa taarifa kadri uchunguzi unavyofanyika.
“Baada ya kupata majibu haya ya awali hatua zifuatazo zimeendelea kuchukuliwa ambapo hatua ya kwanza tunachukua sampuli,tunapeleka maabara kwa ajili ya uchunguzi ili kuweza kutambua sababu ya maji kuwa meusi na aina gani ya mafuta ambayo yameweza kuonekana kwenye maji na chanzo cha mafuta hayo ni nini?,” amesema Shinhu.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi