December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodi ya Wadhamini NSSF yazinduliwa

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama (wanne kushoto) akimkabidhi kitendea kazi, Katibu wa Bodi ya Wadhamini Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, (NSSF) ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Masha Mshomba. ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi wa Bodi hiyo kweny ukumbi wa NSSF mjini Morogoro leo. Wengine pichani ni Mwenyekti mpya wa Bodi hiyo, Balozi Ali Idi Siwa, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigela, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Profesa Jamal Katundu

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amezindua Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, (NSSF) kwenye hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa NSSF Mafao House mjini Morogoro Januari 8, 2022.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo ni Balozi Ali Idi Siwa ambaye aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo kwa kipindi kingine cha miaka mitatu.

Akizungumza na Wajumbe wa Bodi hiyo, Waziri aliwapongeza kwa kuaminiwa na kuwataka wawe wasimamizi wazuri wa Mfuko kwa kushirikiana na Menejimenti.

“Nichukue nafasi hii kuwapongeza Wajumbe walioteuliwa lakini nimpongeze sana mwenyekiti wa bodi ambaye amerudi tena kuongoza bodi hii kwa kipindi kingine cha awamu ya pili cha miaka mitatu.” Alisema na kuongeza………..:Wenzangu Mfuko huu si mdogo hesabu za Disemba 2021 thamani imepanda hadi Trilioni 5.4 wakati huo bodi iliyokuwa ikiongoza Mfuko ilikuwa chini ya Balozi Siwa, hapa ndio tunaona ni kwa sababu gani Mhe. Rais ameona amrudishe kuendelea Kuongoza tena Bodi ya NSSF” Alifafanua.

Alisema matazamio ya Serikali ni kwamba yale yaliyofanyiwa kazi vizuri kwenye Bodi iliyopita, chini ya Bodi hii mpya wanapaswa kuongeza nguvu mara mbili na zaidi ili kwenda mbali zaidi ya hapo Mfuko ulipo na hilo linawezekana.

Aliwakumbusha majukumu ya Bodi kuwa ni kuangalia ustawi na uendelevu wa Mfuko, ambapo moja ya majukumu hayo ambayo yapo kisheria ni pamoja na kuandikisha Wanachama ili kupanua wigo wa uchangiaji ambao thamani ya Mfuko inaongezeka pia.” Alifafanua Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama akizungumza na wajumbe wa Bodi (hawapo pichani)

Aidha Waziri Mhagama alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba ambaye katika kipindi kifupi tangu ateuliwe kuongoza Mfuko huo, amehakikisha kuwaweka wafanyakazi wote kuwa kitu kimoja, timu moja.

“Mahali popote ambapo wafanyakazi ni wamoja tija itapatikana, tumeshuhudia kasi ya kukua kwa Mfuko, lakini utatuzi wa changamoto mbalimbali za Mfuko ambazo ni shirikishi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wanaongea lugha moja na sasa Bodi imeingia wote tutakuwa kitu kimoja.” Alifafanua.

Kwa upande wake, Mwenyekiti huyo mpya wa Bodi, Balozi Ali Idi Siwa alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kwa kipindi kingine cha pili cha miaka mitatu.

“Uteuzi huu na imani hii ni changamoto kubwa kwangu na chachu kubwa ya kunifanya niweze kurudisha imani kwake kwa kufanya kazi kwa nguvu zaidi na ufanisi zaidi.” Alisema.

Pia alimpongeza Waziri kwa uteuzi alioufanya wa wajumbe wa Bodi kwa kuzingatia mahitaji ya taaluma na hana shaka kuwa Bodi imesheheni taaluma zinazohitajika.

Alisema kwa sasas kazi ya Bodi ni moja tu, kutimiza yale ambayo wanapaswa kuyatimiza ikiwa ni pamoja na usimamizi na kutoa mwelekeo.

Mmoja wa wajumbe wa bodi akifuatilia

“Sisi kazi hii tunayokwenda kufanya inapimika, na tuache watu wa aina tatu watupime ambao ni wale wanaotusimamia ambao niwizara, Menejimenti inapofanya tathmini zake za kazi na Wanachama wa Mfuko.” Alibainisha.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba alimshukuru Mhe. Waziri kwa kuzindua Bodi hiyo ambayo alisema imesheheni uzoefu wa kutosha.

”Ninahakika kwa sasa tutakwenda mbele tukijivunia kwa uhakika yale malengo tuliyojiwekea kwenye mikakati yetu ya maendeleo ambayo unaishia 2025 tutayatimiza, sambamba na yale ambayo sisi kama Taasisi tunayopaswa kuyatimiza ambayo yapo kwenye mpango wa taifa wa miaka Mitano unaoishia 2025, ikiwa ni pamoja na maelekezo ambayo Mhe. Rais aliyatoa Bungeni akielezea dira yake yay ale atakayoyafanya katika uongozi wake.” Alisema.

“NSSF inakwenda vizuri, na kama ambavyo unajua tuna wanachama kutoka sekta binafsi ambao kisheria inatupasa kuwa cover wote, lakinipia sharia iliyofanyiwa marejeo 2018 ilitupa mamlaka ya kuwa cover pia Sekta isiyo rasmina katika hii napenda kukuhakikishia kwamba Mfuko unafanya kazi kubwa ili kuhakikisha kwamba matarajio yaku cover Sekta yote isiyo rasmitunaifikia.” Alitoa hakikisho Bw. Mshomba.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Profesa. Jamal Katundu, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigela na Menejimenti ya Mfuko wa NSSF.