November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodi ya ushauri ya Tarura yakagua ujenzi wa barabara ya visiga- zegereni – misugusugu iliyopo mkoani Pwani

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza ujenzi wa barabara ya Visiga – Zegereni- Misugusugu yenye urefu wa Km 12.5 kwa kiwango cha lami iliyopo mkoani Pwani ili kuwezesha malighafi kuingia viwandani kwa urahisi lakini pia kutoa bidhaa viwandani na kupeleka sokoni.

Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi inayofanywa na Bodi ya Ushauri ya TARURA mkoani Pwani, Meneja wa TARURA Wilaya ya Kibaha Mhandisi Samwel Ndoveni alisema kuwa mradi huo wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami unalenga kuhakikisha viwanda vilivyo katika maeneo hayo vinafikika kwa urahisi kipindi chote cha mwaka.

“Barabara hii ni mkombozi kwa wananchi pamoja na wawekezaji maana lengo ni kuhakikisha barabara hii inapitika katika kipindi chote cha mwaka ili malighafi ziingie viwandani urahisi”, alisema Mhandisi Ndoveni.

Kuhusu ubora wa barabara, Mhandisi Ndoveni alifafanua kuwa barabara hiyo inatengenezwa kwa uwezo wa kupitisha magari yenye uzito wa zaidi ya tani 30.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi TARURA Bibi Azimina Mbilinyi alieleza kuwa mradi huo umelenga katika kukuza uchumi wa wananchi na kuwezesha mizigo kuingia na kutoka viwandani kwa urahisi.

Bodi ya Ushauri ya TARURA inaendelea na ukaguzi wa miradi mbalimbali inayo tekelezwa katika Mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.