November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodi ya REA yataka umeme vijijini utumike kuzalisha mali

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Bodi ya Nishati Vijijini (REB) inayosimamia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imetoa wito kwa wananchi walionufaika kwa kupata umeme kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wakala hiyo, kuitumia nishati hiyo kwa shughuli za uzalishaji mali ili kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Janet Mbene ametoa wito huo Septemba 5, mwaka huu jijini Mwanza, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kuhitimisha kikao kazi baina ya Wajumbe wa Bodi na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani humo.

Amesema, mojawapo ya majukumu ya Bodi hiyo ni kuhakikisha kuwa fedha nyingi zinazotolewa na Serikali pamoja na Wafadhili mbalimbali kuwezesha usambazaji umeme vijijini hazipotei bure bali zinaleta manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi walengwa.

Kwa muktadha huo amesema, Bodi inamshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Serikali anayoiongoza, kwa kuendelea kutenga fedha za kuwezesha utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini.

Akieleza zaidi, Mbene amesema ikiwa walengwa na wanufaika wa miradi ya umeme vijijini hawaitumia nishati hiyo kwa shughuli za uzalishaji mali, watakuwa hawaitendei haki Serikali yao badala yake watakuwa wanaisababishia hasara kwa kutotimiza malengo yake.

Msimamizi wa Miradi ya REA Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Ernest Makale (aliyesimama),akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Janet Mbene (Meza Kuu – katikati) na Wajumbe wa Bodi, Mhandisi Styden Rwebangila (kulia kwa Mwenyekiti) na Florian Haule (kushoto kwa Mwenyekiti) wakati wa kikao kazi baina ya Bodi na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani Mwanza, kilichofanyika Mwanza.

“Kazi ya REA ni kupeleka nishati bora vijijini kwa lengo la kuwakomboa wananchi kiuchumi na kuboresha maisha yao na siyo kupeleka mwanga wa taa pekee ambao unaishia kumulika pasipo kubadilisha hali ya maisha ya walengwa,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Bodi amesema wameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini inayoendelea mkoani humo.

Amesema, wakandarasi wengi wamefikia asilimia zaidi ya 80 hali inayotoa matumaini ya kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.

Aidha, amewashukuru watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoani Mwanza kwa ushirikiano ambao wameendelea kuutoa kwa REA katika kusimamia miradi husika.

Vilevile, amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Waratibu wa Miradi ya REA walioko kila Wilaya nchini, kwani uwepo wao umepunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko kutoka kwa viongozi mbalimbali, hususani wa kisiasa kuhusu upatikanaji wa taarifa za maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini katika maeneo yao.

Amewataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi na kutoa ushirikiano mkubwa kwa viongozi hao ambao ni wawakilishi wa wananchi.

Awali, akizungumza katika kikao kazi hicho, Meneja Usimamizi Miradi ya REA, Mhandisi Romanus Lwena alibainisha kuwa jumla ya miradi sita ya umeme vijijini inatekelezwa mkoani Mwanza.

Aliitaja kuwa ni Mradi wa REA III Mzunguko wa Kwanza, REA III Mzunguko wa Pili pamoja na Ujazilizi Awamu ya Pili A.

Mingine ni Mradi wa Upelekaji Umeme kwenye Vituo vya Afya na Visima vya Maji, Miji-Vijiji pamoja na Mradi wa Upelekaji umeme kwenye maeneo ya migodi, viwanda na kilimo.

Kwa upande wake, Mhandisi Miradi (TANESCO) Mkoa wa Mwanza, James Kabasa ameishukuru REA kwa kutekeleza miradi mingi ya umeme vijijini mkoani humo.

Amesema, miradi hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kuwafikia wananchi wengi ambao walikuwa na uhitaji wa umeme. Aidha, ameomba REA iendelee kupeleka miradi mingine mkoani humo ili kuyafikia maeneo mengine zaidi yenye uhitaji.