Na Irene Clemence, Times Majira Online, Dar es Salaam
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu(HESLB) imesema, hadi kufikia Juni mwaka huu, imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi billioni 192 kutoka kwa wakopaji wa bodi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho 44 ya Kimataifa ya Biashara (DITF) maarufu ‘Sabasaba’ , yanayofanyika jijini Dar es salaam, Mkuu wa HESLB, Abdul Razaq Badru amesema, makusanyo ya mikopo hiyo iliyokusanya ni kutoka kwa wakopaji .
Amesema, mwaka 2015 hadi Juni 2020 jumla ya shilingi trilioni 2.6 zimewekezwa kwenye utoaji mikopo kwa wanafunzi, ambayo ni uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya elimu.
“Bodi imewekeza sana kwenye utoaji mikopo na jinsi wanavyorejesha ndivyo tunavyoongeza wakopaji wengi, tunataka wanufaika waongezeke na kila mwenye kufaulu asikose kusoma hasa wale wa familia masikini ambao ndio kipaumbele chetu,”amesema Badru.
Hata hivyo amesema, kwa mwaka huu mpya wa masomo wamejipanga kufika kila mkoa kusaidia wanafunzi jinsi ya kujaza fomu za kuomba mikopo ili kupunguza makosa yanayofanywa na baadhi yao yanayosababisha wengine kukosa mikopo.
Badru amesema, bodi hiyo inatarajia kufungua dirisha la kuomba mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2020/2021 Julai 20 mwaka huu.
Amesema, wameamua kutangaza mapema maandalizi ya kufungua dirisha hilo ili kuwapa muda waombaji kujiandaa ili matokeo ya mitihani yao ya kuhitimu masomo yatokapotoka waombe nafasi za kujiunga na vyuo mbalimbali.
Alibainisha kuwa, mwaka huu wa masomo 2020/2021 serikali imeidhinisha jumla ya sh Bilioni 468, kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi 125,000 wanaosoma wakiwemo wapya 50,000 wanaotarajiwa kupata mkopo mwaka mpya wa masomo.
“Tumekuja sabasaba kuwaambia wazazi na wanafunzi kwamba tupo na dirisha kwa ajili ya kuomba mikopo kwa mwaka mpya wa masomo 2020/2021 tutafungua Julai 20 mwaka huu, amesema Badru.
Amesema, kila mwaka bajeti ya mikopo huongezeka ambapo mwaka jana ilikuwa Sh bilioni 450 na mwaka huu imeongezeka kwa bilioni 18 .
More Stories
Bei za mafuta Novemba 2024,zaendelea Kushuka
TARURA yaomba Mkandarasi aitwe
Ilemela yakusanya bilioni 3.7.robo ya kwanza