December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BMT yaagiza vyama vya michezo kukamilisha usajili

Na Jumbe Ismailly, TimesMajira Online, Singida

BARAZA la Michezo la Taifa (BMT) limevitaka vyama vya michezo yote katika Mkoa wa Singida kuhakikisha vinakamilisha usajili wa kudumu wa vyama vyao na kwani suala la usajili siyo la hiyari bali ni lazima.

Agizo hilo limetolewa na Ofisa Maendeleo ya Michezo wa Manispaa ya Singida, Samweli Mwaikenda wakati wa kufunga mkutano mkuu wa uchaguzi wa Chama cha riadha Mkoa wa Singida uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa huo.

Mwaikenda ambaye pia ni msajili msaidizi wa vyama pamoja na klabu amesisitiza kwamba, Chama kisichosajiliwa kisheria hakiwezi kutambulika na hakitakuwa na faida ya kuendelea kuwepo na kushiriki katika suala lolote linalohusu michezo inayoisimamia.

“Vyama vya michezo siyo ombi ni sheria kwamba ni lazima visajiliwe kwa sababu vikisajiliwa ndipo vinakuwa vinatambulika kwa hiyo ni suala ambalo sisi kama maafisa michezo maanake ni suala ambalo tutaanza nalo,” amesisitiza Mwaikenda.

Kwa mujibu wa msajili msaidizi huyo zoezi la kuhakiki vyama vyote vinasajiliwa kwa kuanzia ngazi ya wilaya ili kuhakikisha vyama vyote vilivyoanza mchakato wa kukamilisha usajili huo vinakamilisha bila mizengwe yeyote ile.

“Nashukuru saa hizi wengi wameshafanya michakato wameshakamilisha katiba,na wengine katiba zimeshaenda kwa msajili” amefafanua Mwaikenda.

Kuhusu vyama visivyozielewa kikamilifu katiba zao, Mwaikenda amesema, BMT itaendelea kutoa elimu kwenye vyama vyote vyenye changamoto ya kuwa na katiba lakini hawawezi kuzitafsiri.