January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BMT wataka wadau kuchukua fomu uchaguzi CHAMIJATA

Na Irene Clemence, TimesMajira Online

BARAZA la Michezo Tanzania (BMT) limewataka wadau mbalimbali wa michezo kujitokeza na kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali katika Chama cha Michezo ya Jadi Tanzania (CHAMIJATA) badala ya kusubiri siku ya mwisho ya mchakato huo utakaofungwa Desemba 13 mwaka huu kuelekea uchaguzi Mkuu utakaofanyika Desemba 19.

Wito huo umetolewa na Ofisa Uhusiano wa BMT, Frank Mdunga ambaye amesema kuwa, wagombea wa nafasi mbalimbali wanapaswa kujitokeza mapema kabla ya mchakato huo kufungwa.

Amesema kuwa, hiyo ni fursa nzuri kwao kugombea nafasi mbalimbali ili waweze kutimiza malengo yao ya kuuendeleza utamaduni wa Mtanzania sambamba na kiutagaza nchi Kimataifa.

“Desemba 19 ndio siku ya uchaguzi lakini zoezi la kuchukua na kurudisha fomu litafungwa rasmi Desemba 13 na kisha kufuatiwa na michakato mingine ikiwemo kukata furaa na kampeni ili ambazo zitawapa fursa wagombea kunadi sera zao za kuhakikisha Taifa linaendelea mbele katika michezo ya jadi, ” amesema Mdunga

Katika uchaguzi huo nafasi zitakazogombaniwa ni pamoja na nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Kaimu Katibu, Mweka Hazini na nafasi nne kwa Wajumbe.

Amesema kuwa, hadi jana tayari wagombea wawili walikuwa wamijitokeza kuchukua fomu na wanataraji wa wadau wengi zaidi wa mchezo huo watajitokeza kabla ya zoezi hilo kufungwa rasmi.

Kwa upande wake David Msuya ambaye amejitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Shirikisho hilo ameahidi kujenga ofisi ya michezo ya asili katika kila Wilaya endapo atafanikiwa kuchaguliwa.

“Nilichukua fomu na tayari nimeirudisha katika ofisi za BMT na kilichonisukuza kuchukua fomu ni uzoefu wangu na ninatakani kuona siku moja tunafikia malengo yetu ya kudumisha ushirikiano na kuhakikisha utamaduni wa Mtanzania unafahamika Kitaifa na ulimwengu kwa ujumla,” amesema Msuya.

Kwa miaka mingi kama mdau wa michezo amekuwa mstari wa mbele kushiriki shughuli za michezo kwa kugawa vifaa mbalimbali katika shule kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa Mkoa.

“Endapo nitapata nafasi hii nitahakikisha utamaduni wa Mtanzania unakuzwa kuanzia ngazi elimu ya msingi kama njia kwa kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Rais Dkt.John Magufuli” amesema Msuya.