February 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Biteko:EWURA yaimarisha utulivu sekta ya nishati

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Tanga

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),imefanikiwa kusimamia huduma za nishati na maji nchini,hali ambayo imechangia kuimarisha utulivu kwenye sekta ya nishati na taifa kwa ujumla.

Hayo yameelezwa na Februari 17, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko,wakati akifungua kikao cha nne cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa EWURA kinachofanyika jijini Tanga.

Ambapo amesema,EWURA,inafanya kazi ya kudhibiti upatikanaji wa huduma za uhakika za umeme na mafuta nchini kwa ufanisi,hali hiyo ambayo imeleta utulivu kwenye sekta ya nishati nchini.

“Mmerahisiha mazingira ya uwekezaji kwenye CNG, vituo vya mafuta vijijini na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwenye nishati safi ya kupikia, nawapongeza,”amesema Biteko.

Dkt. Biteko,ameisisitiza EWURA kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia,kuweka mazingira wezeshi ya kiudhibiti kuhusu ajenda ya misheni 300 ya umeme,kuwasimamia watoa huduma wanaodhibitiwa kuhakikisha wanakuwa na mikataba ya huduma kwa mteja inayotekelezeka.

Pia ameitaka EWURA, kuhakikisha inaendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara ya mafuta nchini, na kushirikisha wadau na watoa huduma wanaodhibitiwa kwenye maamuzi ya kiudhibiti ili utekelezaji wake uwe na tija.

Sanjari na hayo ameitaka EWURA kufanya tafiti za kina kuhusu huduma zinazodhibitiwa ili kubaini maeneo yanayohitaji kutiliwa mkazo,pamoja na kufanya kazi kwa weledi na kufuata sheria ikiwamo kupokea hoja za wanaokosoa utendaji wa taasisi ili kuisaidia kujitathmini na kuboresha zaidi utendaji wake.