-Kituo Kujaza gesi kwenye magari 800 kwa siku
-Serikali kuwapa ushirikiano wawekezaji
Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo amezindua kituo cha kwanza cha kisasa cha kujazia gesi asilia kwenye magari na karakana ya kuweka mfumo wa gesi asilia ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa mipango ya Serikali kuchochea matumizi ya gesi asilia kama nishati safi na salama kwa mazingira.
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam tarehe 11 Novemba, 2023 na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, Balozi Sherif Ismail wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Balozi Isaac Njenga wa Jamhuri ya Kenya, Balozi Fred Mwesigye wa Jamhuri ya Uganda, Mha. Felchesmi Mramba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya TAQA, Pakin Kafafy.
Dkt. Biteko amesema kuwa, kujengwa kwa kituo hicho na TAQA Arabia na washirika wao JCG Oil & Gas niutekelezaji wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa na maono ya kuleta wawekezaji nchini wakiwemo wanaowekeza kwenye Sekta ya Nishati, hivyo ameahidi kuwa Wizara itafanyia maelekezo yake ili kutekeleza maono yake.
Dkt. Biteko amesema kuwa, Serikali inaweka msukumo mkubwa kwenye matumizi ya gesi ya asilia yakiwemo magari, mitambo ya viwandani, hivyo kuzinduliwa kwa kituo hicho ni kuonesha azma ya Serikali ya kuhakikisha kuwa Gesi inayopatikana Tanzania inatumika ndani ya nchi kwanza.
Amesema kituo hicho kitajaza gesi kwenye magari 800 kwa siku na kina pampu sita zitakazojaza gesi kwenye magari sita kwa maramoja ambapo ujazaji wa gari moja utakuwa ni wa dakika tatu hivyo hicho ni kituo kikubwa kitakachosaidia kubadilisha magari na kufanya yatumie gesi badala ya mafuta pekee.
Amesema Kampuni hiyo inatarajia kujenga vituo 12 vya CNG jijini Dar es Salaam ili kuwa na vituo vingi zaidi vya kujazia gesi kwenye magari.
Ameongeza kuwa, kampuni hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wapo kwenye majadiliano ili kujenga vituo vidogo vya Gesi ya Kusindika (LNG) ili kuweza kutoa Gesi jijini Dar es Salaam na kupeleka kwenye mikoa mbalimbali ili nayo iweze kujaza gesi hiyo kwenye magari..
Amesema kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono katika uwekezaji wao ili kuchochea ukuaji wa nishati nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo ameishukuru Wizara ya Nishati kwa kutekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya usambazaji nishati katika maeneo yote ikiwemo gesi asilia.
Amesema kuwa Wilaya ya Ilala, inaona faraja kufunguliwa kwa kituo wilayani humo kutokana na kuwa kitovu cha Mkoa wa Dar es Salaam kwani Wilaya hiyo ina wananchi wasiopungua milioni 1.6 ukilinganisha na idadi yote ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao jumla yao ni milioni 5.3.
Matukio mbalimbali katika picha wakati wa uzinduzi wa kituo hicho
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango