Na Mwandishi wetu, Timesmajira
NAIBU Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Doto Biteko, ameagiza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kuweka utaratibu wa kuwatambua na kuwatuza wahandisi wanaotekeleza miradi kwa viwango vya juu vya ubora, ili kuongeza ushindani wa kitaaluma na kuchochea ufanisi katika sekta ya uhandisi nchini.
Pia amewataka wahandisi kutoruhusu leseni zao kutumika na watu wasiosajiliwa kwani kufanya hivyo wanaokiuka maadili ya taaluma, na kinyume na viapo vya taaluma hiyo na inahatarisha heshima ya uhandisi nchini.

Akifungua Maadhimisho ya 22 ya Siku ya Wahandisi yaliyofanyika jijini Dar es Salaam mapema leo Septemba 25, 2025 kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ,Dkt. Biteko amesema motisha kwa wahandisi wanaofanya kazi kwa umahiri mkubwa ni njia mojawapo ya kuimarisha nidhamu, ushindani na weledi katika taaluma hiyo muhimu.
“Itakuwa vyema kama tukawa na utaratibu wa kuwatuza wahandisi waliotekeleza miradi kwa ubora mkubwa. Hii itasaidia kuongeza ushindani wa kitaaluma na motisha katika kazi,” amesema
Akizungumzia wahandisi wanaokiuka maadili Dkt biteko amesema ni aibu kwa mhandisi aliyepewa leseni kuiruhusu itumike na watu wasiosajiliwa.
“Hii ni kinyume na maadili na inahatarisha heshima ya taaluma ya uhandisi,” amesema
Amesema kuwa taaluma ya uhandisi ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya taifa, akibainisha kuwa tafiti zinaonesha kuwa kila dola moja inayowekezwa katika sekta hiyo huongeza uzalishaji kwa kati ya dola saba hadi kumi.
“Dunia yote inatambua kuwa taaluma ya uhandisi ni moyo wa maendeleo ya nchi yoyote. Zaidi ya asilimia 70 ya wabunifu wa teknolojia wanatoka katika taaluma hii. Sekta kama nishati na akili bandia ni mifano ya wazi ya mchango wa wahandisi,” amesema.

Dkt. Biteko pia aliitaka ERB kuweka mikakati ya kuwawezesha wahandisi vijana na chipukizi, badala ya kuwakandamiza au kuwazuia kupata nafasi za kukua kitaaluma. Alisema ni jukumu la bodi hiyo kuhakikisha wanawajengea mazingira bora ya kujifunza, kujifunua, na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya miradi ya kitaifa.
“Ni muhimu sana kuwawezesha wahandisi vijana ili baadaye waweze kusimamia miradi mikubwa kama ilivyo kwa wakongwe. Bodi ina jukumu la kuhakikisha wanawainua na kushughulikia changamoto zao,” alisisitiza.
Kwa upande mwingine, aliitaka ERB kuwafuata wahandisi walioko kazini, kuwajengea matumaini, na kuwaonesha kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wao katika maendeleo ya taifa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ERB, Mhandisi Wakili Menye Mangu, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwaamini na kuwashirikisha wahandisi wazawa katika miradi mbalimbali ya kimkakati.
“Kama bodi, tumejipanga kuanzisha utaratibu wa kutoa tuzo kwa wahandisi wanaoshiriki kwenye miradi mikubwa, kama njia ya kutoa motisha kwa kazi nzuri wanayoifanya,” amesema Mhandisi Mangu.
Aliongeza kuwa hadi sasa ERB imesajili wahandisi 44,000 huku lengo la mwaka huu likiwa ni kufikia usajili wa wahandisi 80,000 .
Naye Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ambaye amesema jumla ya washiriki 4,000 kutoka mataifa mbalimbali walihudhuria hafla hiyo na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa wahandisi, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa viwango vya kimataifa.



More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi