Na Mutta Robert, TimesMajira Online, Geita
WAZIRI wa Madini, Doto Biteko amekanusha taarifa zinazoenezwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuwa Kampuni ya Madini ya Barrick Gold Corporation ilisaini Mkataba mwaka 2017 na kusaini mkataba mwingine mwaka 2020.
Akitoa ufafanuzi juu ya jambo hilo, Waziri Biteko amesema kuwa, Barrick ina mkataba mmoja tu uliosainiwa na Tanzania ambao ulisainiwa Januari 24 mwaka huu hivyo hakuna mkataba wowote uliosainiwa baina ya Serikali ya Tanzania na Barrick Gold Corporation mwaka 2017 kama watu wanavyo jaribu kupotosha umma .
Biteko ametoa ufafanuzi huo mjini Geita wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ambao walitaka kupata ufafanuzi kuhusu habari zilizoenea kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuhusu serikali na kampuni ya Barrick kuwepo utata kwenye mikataba .
Kwa mujibu wa Biteko, Wizara ya Madini baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 na majadiliano na kampuni hiyo, mabadiliko kadhaa yalifanyika katika mikataba na hadi sasa yanatekelezwa na kampuni husika.
Baadhi ya masharti ambayo yapo kwenye mkataba huo ni kufungua akaunti za Barrick Gold Corporation ndani ya Tanzania jambo ambalo Kampuni hiyo imetekeleza kwa vitendo.
Pia walikubaliana kuwa endapo Kampuni hiyo imepata mkopo nje ya nchi ni lazima kusajiliwa hapa Tanzania kwenye Benki Kuu (BOT).
Kuhusu suala la kusafirisha makinikia, Waziri Biteko ameeleza kuwa, zamani yalikuwa yanasafirishwa hadi eneo la kuyeyushia (Smelting point) lakini kwasasa mnunuzi analeta fedha Tanzania na kuja kununulia hapa nchini.
Amesema, sekta ya madini imepata mafanikio makubwa katika kipindi kifupi na kuleta maendeleo makubwa serikalini katika ukuaji wa kisekta, kuingiza fedha za kigeni nchi, kuongezeka mapato yanayotokana na madini kwa mwaka kulinganisha na sekta nyingine.
Hadi sasa sekta hiyo imekua kwa asilimia 17.7, imeongoza kwa kusafirisha bidhaa zote nje ya nchi kwani sekta ya madini inasafirisha asilimia 51.9 na mapato kutokana na madini kuongezeka kwa mwaka kutoka bilioni 168 hadi bilioni 520 kwa mwaka.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi