March 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Biteko: Afrika tunayapa kipaumbele matumizi Nishati Safi kukabiliana mabadiliko ya Tabia nchi

*Asema Sera na Sheria zinazowekwa zinahimiza matumizi ya Nishati Safi

*Afungua Mkutano wa Awali EAPCE’25

*Ataka utumike kujadili mipango kuhusu matumizi Nishati Safi

*Ataka mkazo kuwekwa kwenye Nishati Safi ya Kupikia, matumizi ya kuni na mkaa bado ni makubwa

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema licha ya Bara la Afrika kuwa na mchango mdogo katika uchafuzi wa hali ya hewa, nchi za Afrika bado zimekuwa mstari wa mbele katika kuendesha ajenda ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuijumuisha katika mifumo yao ya kisheria.

Lakini pia, na udhibiti ikiwemo ya kuhakikisha kuwa nchi zinahama kutoka kwenye matumizi ya nishati chafu na kutumia nishati safi ili kuiepusha dunia na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Dkt. Biteko ameyasema hayo leo tarehe 4 Machi, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Mkutano wa awali kuelekea Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25) litakaloanza rasmi kesho.

Mkutano huo wa awali ulilenga kujadili mipango na mikakati itakayopelekea matumizi ya nishati safi katika maeneo mbalimbali ikiwemo kupikia na vyombo vya usafiri (CNG).

Amesema mkutano wa EAPCE’ 25 ni jukwaa muhimu kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na wadau wengine kujadili mipango na mikakati kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi hasa ikizingatiwa kwa sasa dunia inapambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa kiasi kikubwa zinachangiwa na shughuli za binadamu huku tafiti za kisayansi zikionesha kuwa viwango vya utoaji wa hewa ya ukaa vimeongezeka kwa kiasi kikubwa tangu kufanyika kwa Mapinduzi ya Viwanda.

“Nataka nichukue nafasi hii kuwaomba wote muutumie mkutano huu kujadili masuala ambayo yatatufanya sisi wana Afrika Mashariki, tuweze kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati isiyokuwa safi kwenda kwenye matumizi ya nishati iliyosafi.

“Lazima mtambue kwamba mkutano huu wa awali haujatokea kwa bahati mbaya, kama jamii tunayo kazi ya kufanya ya kutoka kwenye matumizi ya nishati isiyo safi kwenda matumizi ya nishati safi.” Amesisitiza Dkt.Biteko.

Ameeleza kuwa, sheria nyingi zinazopitishwa kwa sasa barani Afrika zinahimiza uchumi wa kijani, kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kuwa na maendeleo endelevu ambapo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa upande wake imeandaa Sera ya Mabadiliko ya Tabianchi ikiwa ni uthibitisho wa dhamira ya kanda hiyo katika kushughulikia tatizo la mabadiliko ya tabia nchi na kuhimiza matumizi ya nishati safi.

Ametaja baadhi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi kuwa ni pamoja na ukame mkali, mafuriko, kupotea kwa viumbe hai, kupungua kwa vyanzo vya maji safi, kuyeyuka kwa barafu, na ongezeko la magonjwa yanayohusiana na tabianchi kama vile saratani ya ngozi.

Dkt.Biteko ameeleza kuwa, suala la mabadiliko ya tabia nchi linatiliwa mkazo pia katika ngazi ya dunia na hii imepelekea kuwepo kwa mikataba mbalimbali ya kimataifa ukiwemo wa Kyoto, Montreal na Paris ambapo nchi zilizoendelea na zinazoendelea zinaandaa na kutekeleza mikakati inayohusiana na tabianchi ikiwemo kujikita katika matumizi ya nishati safi zisizochafua mazingira ikiwemo Gesi Asilia.

Kuhusu upatikanaji umeme amesema, Afrika ndiyo Bara linalokabiliwa na upungufu mkubwa wa nishati duniani, ambapo asilimia 75 ya watu wanaokosa nishati duniani wanapatikana barani humo lakini juhudi zinafanyika ili kuwezesha upatikanaji wa nishati na hili lilithibitishwa kupitia Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati uliofanyika Tanzania Januari mwaka huu ambao uliweka mikakati ya kuongeza upatikanaji wa umeme kwa Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030 ambayo ni hatua muhimu kuelekea mabadiliko ya kinishati.

Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia amesema, mabadiliko yanahitajika ili kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi kwani idadi kubwa ya watu barani Afrika bado wanategemea kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia.

Akitolea mfano nchini Tanzania, takriban asilimia 81 ya kaya zinatumia kuni na mkaa kama vyanzo vyao vikuu vya nishati ya kupikia, hali inayosababisha upotevu wa misitu wa takriban hekta 469,420 kila mwaka.

Akitanabaisha kuwa mwelekeo huo wa kutisha unahitaji hatua za haraka na za pamoja ili kuendeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia barani kote.

Amesema, katika kukabiliana na changamoto hiyo nchini Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni kinara wa ajenda nishati safi ya kupikia kitaifa na kimataifa kwa ujumla amechukua hatua madhubuti kwa kutekeleza Mkakati wa Kitaifa Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034).

Makakati huo unalenga kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Aidha, amesema matumizi ya gesi asilia kama nishati ya kuendeshea vyombo vya usafiri pia ni muhimu katika kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi akieleza kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha mazingira kwa wawekezaji binafsi kushiriki katika ujenzi wa Vituo vya Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG) na kuboresha sera na mifumo ya udhibiti.

Naibu Waziri Nishati, Judith Kapinga kwa upande wake amesema mkutano huo wa awali unaweka msingi wa Kongamano la 11 la Mafuta kwa Nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki litakaloanza kesho Machi 05, 2025.

“Siku ya leo kutakuwa na mada mbalimbali zitakazozungumzwa, ambazo zitakuwa na majadiliano yatakayoweka msingi kwa ajili ya mkutano mkuu utakaoanza kesho na kufanyika kwa siku tatu.

“Mkutano huu ni muhimu katika kuwaweka wadau pamoja na kujadiliana masuala ya msingi ambayo yatazisaidia Nchi za jumuia ya Afrika Mashariki katika Sekta ya Mafuta na Gesi,” Amesema Kapinga.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema mkutano huo wa Mafuta na Gesi unaenda sambamba na Maonesho ya bidhaa za mafuta na gesi pamoja na kazi mbalimbali zinazofanyika katika sekta miongoni mwa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ameeleza kuwa, Mkutano umelenga kuangalia namna bora ya kuhama kutoka kwenye nishati zinazochafua mazingira kwenda kwenye nishati safi zisizochafua mazingira ikiwa ni kampeni ya dunia ambayo imetokana na malengo ya dunia ya kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2050 hadi 2060 dunia iwe imeweza kuhamia kwenye nishati safi kwa kiasi kikubwa.

Mhandisi Mramba ameeleza kuwa, katika mkutano huo nchi zitapata nafasi ya kuelezea maendeleo waliyofanya katika eneo la mafuta na gesi ambapo Makatibu Wakuu na Mawaziri watazungumza kuhusu mafanikio, mipango na kazi zilizofanyika tangu kufanyika kwa mkutano uliopita wa EAPCE.

Amesema, katika mkutano wa EAPCE’25 wataalam, watafiti na wabunifu mbalimbali watazungumzia ugunduzi wa mafuta na gesi, sehemu ambazo vitalu vinanadiwa na kukaribisha uwekezaji kwa nchi za EAC.