Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KATIKA kuunga mkono juhudi za Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha watanzania wote wanapata huduma ya bima, Britam Insurance Tanzania imetambulisha bima zake mpya za matibabu ‘Afya Care’ na ‘Amani Health,’.
Bima hizo ni mahususi kwa ajili ya kutoa huduma ya afya ya kina na unafuu kwa watu binafsi na familia.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari Agosti 6 mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Britam Insurance Tanzania, Farai Dogo amesema, wana furaha kubwa kutambulisha bima hizo.
“Tunayo furaha kuitambulisha Afya Care na Amani Health, bidhaa ambazo zinaonyesha dhamira yetu ya kutoa huduma bora za bima ya afya kwa wateja wetu.
“Lengo letu ni kuleta utulivu wa akili kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya, na hivyo kuimarisha ustawi wa wateja wetu.
“Amani Health ni bima ya afya mahususi kwa wafanyabiashara, makampuni na vikundi vilivyosajiliwa rasmi. Bima hii inatosheleza angalau wafanyikazi au vikundi kuanzia vitano (5) pamoja na wategemezi wao,” amesema Dogo.
Kwa upande wake, Meneja wa Idara ya Bima ya Afya-Britam Insurance Tanzania, George Mwita amesema Afya Care’ ni bima ya afya ya kipekee kwa ustawi wa mtu binafsi na familia
“Kama wewe unatafuta bima thabiti kwa ajili yako binafsi au familia, bidhaa yetu imuendwa kuhakikisha unapokea huduma bora za afya kwa bei nafuu.
“Bima ya afya ya ‘Amani Health’, imeandaliwa kama mkakati mpana zaidi wa kusaidia ukuaji na maendeleo ya wafanyabiashara mbalimbali nchini Tanzania.
“Bima hizi za afya (Amani na Afya Care) ni mkakati wa kusaidia kazi kubwa anayoifanya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha watanzania wote wanapata huduma ya bima,” amesema Mwita.
Aidha, amesema Bima zote mbili ‘Afya Care’ na ‘Amani Health’ zinatoa huduma ya wagonjwa wa kulazwa (Inpatient) na wagonjwa wasio wa kulazwa (Outpatient) kupitia mtandao wao wa watoa huduma za matibabu kwa watu binafsi, vikundi na familia.
Vilevile amesema, Faida zimeundwa maalum kwa machaguo mbalimbali na kutoa viwango tofauti vya faida.
“Chaguo hizi zinatokana na viwango vitatu – POA, IMARA, na SUPER – kwa bei ya chini kama TZS 370,000. Faida za ziada zinazopatikana ni pamoja na Meno, Uzazi, Macho, Mkono wa Pole, na Urejeshaji wa mabaki.
“Huduma za nje ya nchi hutolewa katika nchi zote ambako Bima ya Britam inafanya kazi. Kenya, Uganda, Rwanda, Msumbiji na Sudan Kusini. Huduma za kimataifa na za rufaa zinatolewa ndani ya Afrika Mashariki na India,” amesema.
More Stories
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya