Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa kiasi cha shilingi bilioni 7, kwa ajili ya kuwawezesha vijana 308,kutekeleza miradi waliobuni wenyewe ikiwemo ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.
Vijana hao ni kati ya 486,wanufaika wa programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT-Uvuvi)waliopata mafunzo kwa vitendo ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji,ambapo mitaji hiyo inatolewa kwa njia ya mkopo wenye masharti nafuu.

Akizungumza Machi 7,2026, Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana,Dkt.Joel Nanauka,wakati alikabidhi hundi ya mkopo huo katika uzinduzi wa kukabidhi mitaji kwa vijana hao iliofanyika mkoani Mwanza,amesema mikopo hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali za kuwawezesha vijana kujiajiri na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi kupitia sekta ya uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji.
Pia kutatua changamoto ya ajira kwa vijana ambapo amesema,idadi ya vijana Tanzania wenye umri wa miaka 15 – 35, inakadiriwa kuwa milioni 20.6 sawa na asilimia 34.4 ya idadi ya watu wote nchini.Takribani vijana milioni 1 huhitimu mafunzo mbalimbali kila mwaka,lakini wanaopata ajira katika sekta ya umma ni takribani vijana 40,000 na sekta binafsi 350,000.
Kwa upande wa sekta za mifugo na uvuvi, takribani vijana 1,975 wanahitimu mafunzo katika ngazi ya astashahada, stashahada na shahada kila mwaka,kati yao asilimia 9.5 ya wahitimu katika fani za mifugo na asilimia 23 ya wahitimu katika fani za uvuvi na ukuzaji viumbe maji ndiyo wanaajiriwa serikalini.
Dkt.Nanauka,amesema,kutokana na hali hiyo imeisukuma serikali kufikiria mbinu mbadala ya kuwezesha vijana kujiajiri ili kukabiliana na changamoto ya ajira.
“Kiasi hiki cha bilioni 7, ninachokikabidhi leo kitawezesha vijana 308 ambao niwahitimu wa BBT-Uvuvi kutekeleza miradi ya ufugaji wa samaki kwa vizimba, ufugaji wa jongoo bahari, unenepeshaji wa kaa na kilimo cha mwani. Fedha hizi zinatolewa kama mikopo ya masharti nafuu ya vifaa na pembejeo muhimu za ukuzaji viumbe maji pamoja na posho ya kujikimu,” amesema Dkt. Nanauka

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Uvuvi,Profesa Mohamed Sheikh amesema,kati ya vijana 308 watakaowezeshwa kupitia fedha hizo vijana 160 watatekeleza miradi ya ufugaji wa samaki kwenye vizimba ambao kila mmoja atapatiwa kizimba kimoja kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara.Huku vijana 148 watatekeleza miradi ya ufugaji wa jongoo bahari, kilimo cha mwani pamoja na unenepeshaji wa kaa.
Profesa Sheikh, amesema vizimba ambavyo Waziri huyo ameviona vina uwezo wa kuchukua hadi vifaranga 11,500 na kuzalisha wastani wa tani 3.5 kwa kizimba,katika kipindi cha miezi 7 kwa gharama ya shilingi milioni 17.2, ikiwa samaki hao watauzwa kwa bei ya wastani wa shilingi 7,500.
“Hivyo itazalisha kiasi cha shilingi milioni 26.250 ukitoa gharama, inakuwa sawa na faida ya shilingi milioni 9.0, katika mzunguko wa kwanza, faida hii inaongezeka katika mizunguko inayofuata,”amesema Profesa Sheikh.
Aidha amesema Wizara hiyo ya Mifugo na Uvuvi,inapanga kutumia sehemu ya shilingi bilioni 23 ambazo imezipokea kwa ajili ya kuwezesha vijana zitumike kuwezesha vijana wa BBT waliosalia.

Naye Mkurugenzi wa Mipango, Ushauri na Mahusiano ya Taasisi kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB),Mkani Waziri, amesema tangu mikopo hiyo ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ianze kutolewa zaidi ya bilioni 2 zimerudishwa hivyo kutoa nafasi ya wengine kukopeshwa.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo,Erasto Buyekeleo amesema watatekeleza mradi huo kwa ufanisi na kuchangia pato la taifa na kuwa chachu kwa vijana wengi huku Grace Henry,ameiahidi Serikali kuwa watafanya vizuri katika mradi huo ili waweze kuwaajiri vijana wenzao.



More Stories
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI