Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online
SERIKALI imetenga sh. bilioni 48.6 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyuo 29 vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) vya wilaya, ikiwemo chuo cha Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza ambacho kinatarajiwa kukamilika Septemba 30 mwaka huu.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa Chuo hicho.
Alisema fedha za kukamilisha ujenzi wa chuo hicho tayari zimeshatengwa ili kuhakikisha kinamilika kwa wakati uliopangwa na kwamba mafunzo yataanza mara baada ya kukamilika kwa ujenzi huo.
Alisema gharama za ujenzi wa chuo hicho mpaka kukamilika ni sh. bilioni 2.1 na kwamba hadi sasa imeshatumia sh. Bilioni 1.6 huku sh. milioni 500 iliyobaki ikiwa imetengwa katika mwaka wa fedha 2021/22 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa chuo hicho.
“Niwatoe wasiwasi wananchi wa Kwimba kuwa ujenzi huu unakwenda kukamilika kama ulivyopangwa na tutaanza na kozi za muda mfupi kisha Januari mwakani tutaanza kutoa kozi za muda mrefu,” alisema Kipanga.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Kagera, Juliana Magesa ambaye ndiye msimamizi mkuu wa mradi huo alisema mradi una jumla ya majengo 17 yakiwemo mabweni mawili yatakayokuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 144, kati yao 80 wa kiume na 64 wakike.
Alisema mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 62 na inatarajiwa hadi ifikapo Septemba 30, mwaka huu ujenzi huo utakuwa umekamilika ili kutoa fursa kwa vijana wa Wilaya ya Kwimba na maeneo jirani kupata stadi za kazi watakazozitumia kujiajiri na kuajiriwa na hivyo kukuza uchumi wa Wilaya na Taifa kwa ujumla.
Akiongea kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Kwimba, Mbunge wa Wilaya hiyo, Mansoor Shanif aliishukuru Wizara ya Elimu kwa kujibu ndoto ya muda mrefu ya wananchi wa Kwimba ambayo sasa wanaona inaenda kutimia.
Aidha, aliomba Wizara kujenga uzio wa kuzunguka chuo hicho ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mwingiliano.
Naye Katibu Tawala Wilaya ya Kwimba, Nyakia Ally alishukuru Wizara kwa ujenzi wa chuo hicho cha ufundi na alishauri kiwe na mafunzo ya ufundi magari pia ili kuwarahisishia wananchi wa Kwimba ambao huwa inawabidi waende Mwanza mjini ambapo ni umbali wa kilometa 97 ili kupata mafundi wa kutengeneza magari yao.
More Stories
Tanzania,Uturuki kushirikiana kuinua sekta ya utalii nchini
Wanaoficha watoto wenye ulemavu kusakwa
Mawakili Tabora walaani kuziwa kutekeleza majukumu