December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilioni 4 zatengwa kuimarisha miundombinu Jangwani Dar

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

SERIKALI kupitia Mfuko wa Barabara (Road fund) imesema ipo tayari kupitisha kiasi cha sh.bilioni 4 kwa ajili ya kumlipa mkandarasi atakayepatikana ili kuboresha miundombinu ya Jangwani mara baada ya uhakiki wa makisio hayo kukamilika na kujiridhisha.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Arch. Elius Mwakalinga, akifafanua jambo kwa wajumbe wenzie katika ziara yao ya ukaguzi wa miundombinu ya barabara katika jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Bodi ya mfuko huo,Mwenyekiti wa Bodi Joseph Haule, amesema kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha inatatua changamoto hiyo haraka kabla ya mvua za masika kuanza.

“Bodi imeona tatizo hili na tumeliona kama suala la dharura, ndio maana tumekuja hapa kujionea hali halisi ili kutafuta njia sahihi ya kutatua tatizo hili ambalo limekuwa kero kwa muda mrefu”, amesema Mwenyekiti wa Bodi.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), Bw. Octavian Mshiu, akiwaonesha wajumbe wenzake makalvati yaliyopo katika barabara ya Morogoro, eneo la Jangwani, yaliyoathirika kwa kuzibwa na takataka nyingi na hivyo kuruhusu maji kupita kwa kiasi kidogo, jijini Dar es Salaam.

Aidha,Haule alifafanua kuwa kweli tatizo ni kubwa, mfereji una kina kifupi na makalvati mawili makubwa yaliyopo hapo yameziba kabisa.

Ameongeza kuwa nia ya bodi ni kuona wananchi na wasafirishaji wanatumia mindombinu hiyo wakati wote wa mvua na kiangazi.

Kwa upande wake,Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch.Elius Mwakalinga,amesema kuwa Serikali kupitia Wizara yake imeandaa mkakati wa muda mrefu kuhusu miundombinu hiyo ambapo amesema kuwa kwa sasa wataalamu wanafanya usanifu wa kina kwa ajili ya kuja na suluhisho la kudumu ikiwemo ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 300.

Muonekano wa barabara ya Morogoro katika eneo la Jangwani ambalo Serikali imeandaa mkakati wa muda mrefu wa kujenga Daraja lenye urefu wa mita 300 ili kuondoa adha ya wasafiri na wasafirishaji wa jiji la Dar es Salaam hususan katika msimu wa mvua.

Mwakalinga amefafanua kuwa aliagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuhakikisha wanatafuta ufumbuzi wa haraka ikiwemo kutoa mchanga ambao umetuama katika eneo hilo ili kuinusuru miundombinu hiyo.

Naye,Meneja wa TANROADS mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Julius Ngusa, amethibitisha kuwa ofisi yake inaendelea kuhakikisha kuwa michanga inayotuama katika eneo hilo inatolewa kwa wakati ili kuruhusu magari kuweza kupita mara baada ya mvua kunyesha.

Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wametembelea eneo la Jangwani kujionea hali halisi ya miundombinu katika eneo hilo ambayo imekuwa ikiathiriwa na mvua na kusababisha kufunga mawasiliano ya watumiaji wa barabara ya Morogoro hususani eneo hilo kila mwaka.