January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilioni 22 zatengwa kukamilisha ujenzi jengo la Mkemia Mkuu,Dodoma

Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

SERIKALI imetenga jumla ya shilingi bilioni 22 kwaajili ya kutekeleza  na kuimarisha miundombinu ya uchunguzi wa kimaabara kwa  kukamilisha ujenzi wa Jengo la Ofisi na Maabara la Makao Makuu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo, Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt.Fidelis Mafumiko kuhusu utekelezaji wa shughuli na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 ameeleza kuwa fedha hizo pia zitatumika kununua mitambo na vifaa vya kisasa vya kimaabara kwa ajili ya kuendelea kuboresha uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara kwa lengo la kusimikwa kwenye Jengo la Mamlaka Makao Makuu ya Nchi-Dodoma.

Pamoja na hayo amesema wanaendelea kufanya uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara na utoaji wa ushahidi kwenye Mahakama zote nchini ili kuwezesha na kuharakisha upelelezi wa masuala ya jinai yanayohitaji uchunguzi wa kimaabara, na hivyo kuchangia utoaji wa haki kwa wananchi kwa wakati, lengo likiwa la kusimamia utawala wa Sheria.

Kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani, Sura 182.

Wakati huo huo amesema kuwa Serikali kupitia Mamlaka imepanga  Kuimarisha biashara ya kemikali kwa kuendelea kuboresha usimamizi wa uingizaji wa kemikali nchini kwenye maeneo ya mipakani.

“Katika kutekeleza hilo, Mamlaka itaendelea kutoa huduma za ukaguzi wa shehena za kemikali katika maeneo yote ya mipakani kwa saa 24, siku saba kwa wiki”amesema.

Aidha amesema kuwa Mamlaka itaendelea na utaratibu wa kuimarisha Mfumo wa utoaji vibali vya uingizaji wa shehena za mizigo ya kemikali inayotarajiwa kuingizwa nchini.

Hata hivyo amefafanua kuwa hayo yote yatafanyika ili kulinda usalama wa watu na mazingira kwa kuzuia uingizaji usiozingatia sheria, kanuni na taratibu wa kemikali hatarishi zinazoweza kutumika vibaya kama vile silaha za maangamizi na kudhibiti uingizaji wa kemikali zinazoweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya.