January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilioni 2.6 kutumika kutengeneza barabara Ilemela mwaka wa fedha 2023/24

Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Bilioni 2.67 inatarajiwa kutumika katika matengenezo ya barabara za Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini Tanzania (TARURA) Wilaya ya Ilemela Mhandisi Sobe Makonyo akiwasilisha mapendekezo ya bajeti ya mpango wa matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2023/2024 katika Baraza la Madiwani Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

Ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 TARURA Wilaya ya Ilemela imependekeza kujenga Barabara ya Kahama-Igogwe-Isanzu-Kabusungu (Ilemela Hospital road) yenye urefu wa Km 2.0 kwa kiwango cha lami nyepesi.

Pia barabara ya Mkudi yenye urefu wa Km 0.6 kwa kiwango cha mawe kwa kutumia chanzo cha Mfuko wa Maendeleo ya Barabara endapo bajeti hiyo itaridhiwa na kupitishwa katika ngazi za juu.

Mhandisi Sobe ameviainisha vyanzo vikuu vya fedha za matengenezo ya barabara katika utekelezaji wa kazi za matenegezo, ukarabati na ujenzi wa barabara kuwa ni Mfuko wa Matengenezo ya Barabara, Mfuko wa Maendeleo ya Barabara tozo na Jimbo pamoja na wafadhili wengine kama Benki ya Dunia ambao hutekeleza miradi kwa kushirikiana na TARURA.

“Fedha za Mfuko wa Barabara ni fedha kiasi cha bilioni 1.17 kimetengwa kwa ajili ya matengenezo na ujenzi wa barabara huku chanzo cha fedha za tozo kikiwa kimetengewa bilioni 1, na chanzo cha mfuko wa jimbo kimetengewa kiasi cha milioni 500,fedha hizo zikiwa ni kwa ajili ya matengenezo na ujenzi wa barabara katika mwaka wa fedha 2023/2024,”ameeleza Mhandisi Sobe.

Wakichangia bajeti hiyo Madiwani wameshauri kuwa TARURA ijielekeze zaidi katika barabara ambazo zimekua korofi na zenye changamoto za muda mrefu hususani maeneo ya milimani ambapo wameshauri zijengwe barabara za mawe maeneo kama vile kitangiri,Kirumba,Nyamanoro na Ibungilo

“Jiografia ya Ilemela eneo kubwa imetawaliwa na milima, tujipange kwenye ujenzi wa barabara za mawe hasa maeneo ya miinuko kwani barabara za mawe ndio zinadumu kwa kipindi kirefu,”ameeleza Diwani wa Kata ya Kitangiri Donald Ndalo.