Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online -Tanga
Bilioni 190,zimetolewa kwa ajili ya ufadhili wa mradi wa INCLUSIVE CITIES kwa ajili ya kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi ili kuzalisha vijana wanaohitajika kwenye soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Fedha hizo zimotolewa na Umoja wa Ulaya kwa kupshirikiana na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ubeligiji (ENABEL), kwa ajili ya kutekeleza mradi huo katika Halmashauri za Tanga, Ilemela na Nyamagana(Mwanza) pamoja na Chakechake Pemba,huku Mkoa wa Tanga zaidi ya vijana 350 wanatarajiwa kunufaika.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga ,Balozi Dkt. Batilda Buriani,ametaka mchakato wa kuwapata walengwa ufanyike haraka na kutoa kipaumbele kwa vijana wenye hamu ya kupata mafunzo, ambao baada ya hapo wataweza kutumia utaalamu walioupata kujikwamua kiuchumi hususani waliotoka kwenye familia zisizo na uwezo kiuchumi.
Amesema misingi ya Baba wa Taifa na dhana ya ujamaa wa kujitegemea ilikuwa ni kupitia mifumo ya vyuo vya ufundi lakini na shule za amali ambazo sasa serikali imezirudisha zitawakomboa vijana,kwa sababu watatoka wakiwa na maarifa ya jinsi ya kumudu mazingira.
Mshauri Mtaalamu wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ubeligiji ENABEL,Tomas Aikaruwa, amesema,jijini Tanga mradi huo utawanufaisha zaidi ya vijana 350 kati yao asilimia 50 ni wanawake.
Amesema Umoja wa Ulaya kupitia Green City chini ya mpango wa SASA, watafanya kazi na Serikali ili kuchangia kwenye mikoa ya Tanga,Mwanza na Pemba, lengo ni kuboresha maisha ya watanzania kwenye miji hiyo mitatu kwa kuboresha miundombinu inayozingatia mabadiliko ya tabianchi.

Amewataja wadau ambao watatekeleza mradu huo ni VETA ikiwemo Pemba na Sido Tanga na Mwanza pamoja na sekta binafsi ambazo zinapatikana kwenye mikoa hiyo mitatu chini ya uangalizi wa Halmashauri zinazopatikana kwenye mikoa hiyo Tanga,Mwanza (Ilemela na Nyamagana) na Chakechake Pemba.
Pia amesema ujuzi ni dhana muhimu katika kipindi hiki hasa cha mabadiliko ya mitaala ya elimu,hivyo wanategemea kuibua na kutengeneza ajira na kuimarisha zilizopo ili ziwe na tija kwenye maeneo husika.
“Maeneo tunayotazamia kuyafikia ni utumiaji huduma za kibiashara,kifedha na uwekezaji,pia kuwe na ubora na mafunzo ya ujuzi yanayotolewa na taasisi zilizotajwa, yanayozingata mahitaji ya sasa,ujasiriamali na bajeti ya shughuli ambayo ni bilioni 190,ambapo mradi huo ulianza mwaka 2022 na utakwenda mpaka mwaka 2027,”.
Mkuu wa Chuo cha VETA mkoani Tanga,Gidioni Lairumbe,amesema,programu hiyo ni kuwaandaa na kuwajengea uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa vijana 150 wasio na ujuzi kabisa katika fani mbalimbali.
Amezitaja fani hizo kuwa ni usindikaji na uandaaji wa chakula,umeme wa jua(solar),uchomeleaji na uungaji wa vyuma,matengenezo ya pikipiki za umeme,simu za mkononi pamoja na utengenezaji wa mkaa mbadala ikiwemo mpango wa kuwapa ujuzi vijana walio sokoni ambao utawagusa vijana 150 ukilenga asilimia 50 ya wanawake katika fani.
“Lengo kuu la mradi huu ni kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi kwa kuzalisha wahitimu wanaohitajika katika soko la ajira,na kuifanya VETA Tanga kuwa kituo cha umahiri wa utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi katika sekta husika,”.

More Stories
Waziri Mkuu kuzindua Kampeni ya msaada wa kisheria Dar
Makongoro aielekeza Halmashauri ya Nkasi hoja za kufanyiwa kazi haraka
Zaidi ya bilioni 10.5 zatumika kutekeleza miradi ya maendeleo Kata ya EndiamtuÂ