January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilionea Laizer akabidhi shule ya msingi,atoa ushauri Sabasaba

Na David John,TimesMajira Online, Dar

SANINIU Laizer ambaye hivi karibuni aligeuka kuwa bilionea baada ya kupata mawe ya madini ya Tanzanite amewashauri Watanzania kujenga tabia ya kusaidia jamii inayowazunguka pindi wanapopata mafanikio kwani kufanya hivyo kunaongeza baraka katika shughuli zako.

Leizer ameyasema hayo leo kupitia Maonyesho ya Kimataifa ya 45 ya Sabasaba ambayo yanaendelea wilayani Temeke ambapo amesema kuwa anajisikia faraja sana kwamba anakuwa sehemu ya wadau wanaotambua changamoto zilizopo kwenye jamii hususani wilayani kwake Simanjiro.

Amesema kuwa kutokana na kipato anachokipata kupitia shughuli zake za madini amekabidhi shule ya msingi yenye vyumba saba, nyumba za walimu mbili pamoja na matundu ya vyoo kumi kwa uongozi wa Serikali ya wilaya hiyo.

Ameongeza kuwa kwa kutambua mchango wake huo kwenye sekta ya elimu shule hiyo imepewa jina lake la Saniniu na imejengwa katika Kijiji Cha Naepo kilichopo Kata ya Naisinyai wilayani humo ambapo imetumia zaidi ya shilingi milioni 466 hadi kukamilika kwake.

Laizer ambaye amekuwa kivutio kwenye maonyesho hayo ya Sabasaba kutoka na ushiriki wake mwaka huu huku Banda la Sekta ya Madini likipambwa na picha za bilionea huyo wa Madini ya Tanzanite nchini.

Laizer amesema maonyesho ni mazuri na kubwa zaidi amekuwa akishirikiana vizuri na serikali na ndio maana yupo bega kwa bega na amekuwa akisaidia pindi anapopata fursa ya kufanya hivyo .

“Wakati mwingine kusaidia kunahitaji uzalendo ,upendo thabiti dhidi ya Taifa lako lakini kubwa zaidi kujitoa hivyo nashukuru kwa kufanikisha ujenzi wa shule hiyo ambayo kimsingi niliaza kuijenga mwaka 2017,”amesema Leizera wakati akihojiana na waandishi wa habari kwenye maonyesho hayo.

Saniniu Laizer akitoa ushauri kwa wananchi waliofika kutembelea katika banda lake katika Maonesho ya Sabasaba

Akizungumzia ushirikiano wake na jamii Laizer amesema kuna ushirikiano mzuri na ni yake ni kuisaidia jamii kadri anavyojaliwa na Mwenyezi Mungu na si vinginevyo.

Katika hatua nyingine Bilionea Laizer ameipongeza Wizara ya Madini kwa ushirikiano mkubwa wanaompatia hali ambayo imewezesha kufikia hatua aliyonayo na kwamba ataendelea kushirikiana na Serikali katika kuunga mkono juhudi zake kadri atakavyokuwa anabarikiwa

Katika kipindi hiki cha Maonyesho ya Kimataifa ya Sabasaba amewataka Watanzania kujitokeza Kwa wingi ili kupata elimu ya madini na hasa madini ya Tanzania ambayo yanapatikana nchini tu na wafike kwenye Banda la Wizara ya Madini watapata elimu zaidi.