January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bil 1.8 kujenga madarasa Tabora

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

HALMASHAURI ya manispaa Tabora imempongeza Rais wa awamu ya sita Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia kiasi cha sh bil 1.89 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika shule za msingi.

Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo jana, Mstahiki Meya wa manispaa hiyo Ramadhan Kapela amesema fedha hizo zimekuja wakati mwafaka kwani miundombinu ya shule nyingi imechakaa sana.

Alisema fedha za mradi huo zitasaidia sana kuboresha miundombinu ya shule za msingi katika manispaa hiyo ikiwemo kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji hivyo kuwezesha watoto wote kupata nafasi ya kukaa darasani.

Kapela alibainisha kuwa takribani vyumba vya madarasa 49 vitajengwa katika shule mbalimbali na matundu ya vyoo 64 hali itakayochochea maboresho makubwa ya sekta hiyo hivyo kuongeza kiwango cha ufaulu.

Alitaja baadhi ya shule zitakazonufaika na mradi huo kuwa ni shule ya msingi Chemchem ambapo vitajengwa vyumba 2 vya darasa la awali na matundu 6 ya vyoo kwa gharama ya sh mil 71.8.

Shule ya msingi Izenga itapata vyumba 4 vya madarasa na matundu 3 ya vyoo kwa gharama ya sh mil 110, Kalunde vitajengwa vyumba 3 vya madarasa na matundu 3 ya vyoo kwa gharama ya sh mil 84.6.

Kizigo shule ya msingi watapata vyumba 2 vya madarasa na matundu 3 ya vyoo kwa gharama ya sh mil 58.6 na Magereza watajengewa darasa la awali la mfano, vyumba 14 vya madarasa na matundu 18 vya vyoo kwa sh mil 561.1.

Shule ya Mabatini litajengwa darasa la awali la mfano, vyumba 7 vya madarasa na matundu 10 ya vyoo kwa gharama ya sh mil 361.5 na shule ya msingi majengo watajengewa vyumba 3 vya madarasa na vyumba 3 vya vyoo kwa sh mil 84.6.

Nyingine ni shule ya msingi Miyemba ambayo itajengewa darasa la awali la mfano, vyumba vya madarasa 14 na matundu ya vyoo 18 na vyote vitajengwa kwa gharama ya sh mil 561.1

Kaimu Mkurugenzi wa manispaa hiyo Neema Kapesa alisema mradi huo ni muhimu sana kwani utapunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika shule nyingi hivyo kuinua kuinua kiwango cha elimu katika shule hizo.

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa Tabora ambaye pia ni diwani wa kata ya Isevya, Ramadhani Kapela akiongea katika moja ya vikao vya baraza la madiwani wa halmashauri hiyo hivi karibuni. Picha na Allan Vicen.