Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Tanganyika
Wakala wa Barabara za Vijiji na Mijini (TARURA) inaendelea na ujenzi wa daraja la Ifinsi na makalvati saba kwenye eneo la Mbunga ya urefu wa mita 500 katika barabara ya km 14 kutoka kijiji cha Kambanga hadi kitongoji cha Ifinsi kijiji cha Vikonge kata ya Tongwe wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi.
Ujenzi wa mradi huo unatokana na kata ya Tongwe kuwa na wakazi 48,079 kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) na kuwa eneo linalokaliwa na watu wengi kuliko kata zote wilayani humo hivyo serikali kuona umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya barabara ili kukuza maendeleo.
Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi,Onesmo Buswelu amesema hayo ofisi kwake baada ya kumaliza kukagua ujenzi wa mradi huo wenye thamani ya bilioni 1.5 ambapo amesema Vikonge,Bugwe,Igalukilo na Maghorofani ni vijiji ambavyo ni kitovu cha biashara ya mazao ya kilimo ambapo serikali imeona vema kujenga mindombinu wezeshi kwa wananchi.
Ameeleza licha ya eneo la Ifinsi kukua kwa kasi kwa sababu za kijiografia za kuwa na bonde kubwa la mto Mnyamasi na serikali kuwekeza zaidi kutoa mbolea ya ruzuku kwa wakulima imekuwa chachu ya uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo lakini wakishindwa kupata bei nzuri ya mazao kutokana na ubovu wa daraja ambalo lingewasaidia kusafirisha mazao.
“Mradi huu ni wa kimkakati,kiuchumi lakini kijamii kwa sababu unagusa mahitaji yote ya uchumi,jamii na kisiasa,wanasiasa wengine wanapenda kuisema serikali hapa haijapafanyia kazi lakini wanatakiwa waone sasa serikali inagusa hadi vijijini na vitongoji kuweka miundombinu inayopelekea uchumi wetu ukue,”amesema.
Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijiji na Mijini (TARURA) Wilaya ya Tanganyika,Mhadisi Nolasco Kamasho amesema mradi wa daraja la Ifisi na makalvati umefikia asilimia 87 ukiwa umeanza kujengwa Mei,2023 na utakamilika Februari,2024 ukihusisha ujenzi wa tuta na kingo za kuzuia tuta la urefu wa mita 300 utakaozuia tuta kuondolewa na mvua.
Amesema kutokana na ushindanishi wa kimanunuzi,Mkandarasi Hemed Holding Ltd amepewa fedha zaidi ya bilioni 1 na mil 214 ya ujenzi wa daraja hilo pamoja na Mkandarasi Duzenge co ltd amepatiwa zaidi milioni 285 kwa ajili ya kujenga barabara ya Kambanga – Ifinsi ya Km 8 kwa kiwango cha changalawe,kujenga makalvati saba na madaraja ya mawe mawili katika barabara ya Majalila-Nyagantambo na Ifinsi.
Mhadisi Kamasho alieleza baadhi ya faida za ujenzi wa daraja hilo na makalvati pindi yatakapo kamilika ni pamoja na kusaidia wananchi kusafirisha mizigo yao na wenyewe kusafiri bila adha yoyote ambayo awali walitumia daraja la miti kuvuka.
“Magari ya mizigo yalikuwa hayapiti watu walikuwa wakitoa gunia moja ng’ambo ya kwanza kupeleka ng’ambo ya pili kwa gharama ya Tshs 2,000/= kwa baiskeli na muda mwingine kwa pikipiki na gari zilizokuwa zinaruhusiwa ni ndogo inayobeba watu 16,”amesema.
Adelina Raphael,Mkazi wa Kitongoji cha Ifinsi Kijiji cha Vikonge ameishukuru serikali kwa ujenzi wa daraja na makalvati hayo licha ya faida yake lakini wamepata fursa mpya ya ajira inayosaidia kuwa sehemu ya chanzo cha mapato ya familia zao.
“Nalipwa Tshs 10,000/= kwa siku tizama sasa nimefanya kazi hapa kwa muda wa miezi miwili ninafedha ambazo zinasaidia kuhudumia familia yangu…sio lazima kila kitu nimwachie mume wangu kwenye jukumu la kuhudumia mavazi na chakula,nimekuwa imara na mume wangu ananisifia kwa ujasili wa kufanya kazi,” amesema.
Aidha amewaomba wanawake na wasichana wengine kuchangamkia fursa ya kazi kwenye ujenzi wa daraja Ifinsi kwa kuwa muda ujenzi unaendelea hadi mwakani.
More Stories
Tanzania,Uturuki kushirikiana kuinua sekta ya utalii nchini
Wanaoficha watoto wenye ulemavu kusakwa
Mawakili Tabora walaani kuziwa kutekeleza majukumu