January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani (BFA) wakiwa katika picha ya pamoja, katikati ni Olnjure Marigwa ambaye ameshinda nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho. (Picha na Omary Mngindo).

BFA yapata viongozi wapya

Na Omary Mngindo, TimesMajira Online, Bagamoyo

CHAMA Cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani (BFA), kimepata viongozi wapya watakaokiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Uchaguzi huo umefanyika kwenye ukumbi wa Eagle chini ya Msimamizi Hafidhi Kanyamale akisaidiwa na wajumbe wawili wanaotokea Jimbo la Chalinze Said Mkomwa na Miraji Pazi huku wajumbe wapatao 73 wakishiriki zoezi hilo.

Katika Olnjure Marigwa amechaguliwa Mwenyekiti kupigiwa kura 53 dhidi ya mgombea mwenzake James Manyama ambaye amepigiwa kura 13.

Nafasi ya Makamu Mwenyekiti imekwenda kwa Abdul Pyalla akipata kura 55, huku Salum Kanema akishinda nafasi ya Katibu Mkuu kwa kupata kura 60 akiwa mgombea pekee baada ya aliyetaka kutetea nafasi hiyo Hussein Kipindura kukatiwa rufaa.

Azizi Mwashambwa amepata nafasi ya Katibu Msaidizi akichaguliwa kwa kura 61, Mhazini ni Ibrahimu Gama aliyepata kura 56 akimshinda Ibrahimu Huruka, Mjumbe kuwakilisha Wilaya kwenda Mkoa Ramadhani Rukanga aliyemshinda Kitoro Jonas.

Akizungumza baada ya matokeo hayo, Hafidhi amesema kuwa, zoezi hilo halikushirikisha Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, hivyo amewaagiza viongozi hao kujipanga kwa ajili ya kukamilisha safu hiyo, sanjali na nafasi ya Mwakilishi wa vilabu Wilaya.

“Kwanza niwashukuru wajumbe kwa utulivu mkubwa katika kukamilisha zoezi letu la uchaguzi, niwaombe viongozi mjipange ili kujazia nafasi zilizokuwa wazi kianzia Wajumbe Kamati ya Utendaji na Mwakilishi wa vilabu wilaya,” amesema Kanyamale.

Ofisa Utamaduni Wilaya Vedastus Mziba amewataka viongozi wa klabu na wadau wa mchezo huo wawaunge mkono ili kwa umoja wao waweze kufanikisha kiu ya wana-Bagamoyo katika medani hiyo yenye mashabiki wengi nchini na duniani kwa ujumla.