Na Jackline Martin , TimesMajira Online
BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) kwa kushirikiana na kampuni ya Metro Life Assurance wamezindua Bima Benki yenye lengo la kutoa huduma mbili za Bima ziitwazo ADABIMA na Saccos Schemes Credit Life.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo Mei 17,2024 Jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware amesema kiini cha huduma hizo ni kujenga uelewa wa umuhimu wa elimu katika kujenga kesho bora ya jamii.
kuhusu ADABIMA, Dkt. Baghayo amesema huduma hiyo ni maalum kwa ajili ya ada ya shule inayokamilisha kiu ya mzazi au mlezi kumwona mtoto wake akifanikiwa kwa kupata elimu bora anayostahili ambapo bidhaa hiyo ilithibitishwa na Mamlaka mnamo tarehe 22 Novemba 2023.
“Kama tujuavyo wote, majanga ni jambo lisiloepukika katika maisha yetu. Si mara zote mipango yetu inatimia kama tunavyokusudia. Majanga hutokea katika nyakati tusizotegemea na kuvuruga mipango yetu na familia zetu.”
“ADABIMA ni suluhisho la changamoto hizi za maisha, lakini pia ni ahadi kwa wateja kwamba lolote litakalotokea kampuni yake itasimama pamoja naye kuhakikisha mtoto anasoma na kuhitimu masomo yake bila kadhia yoyote ile.” Amesema Dkt. Baghayo
Kuhusu Saccoss Schemes Credit Life Insurance, Dkt. Baghayo amesema ni huduma ya bima maalum kwa ajili ya wadau wa SACCOS na Vikundi vya huduma ndogo za fedha (micro-finance).
Amesema Mamlaka itahakikisha huduma hiyo inaendelea kuwapa watumiaji usalama wa kifedha, utulivu, kujiamini na amani.
“Wadau hawa wanajenga kesho iliyo bora kwa kuinua uwezo wa watoa mikopo na kuwahakikishia wakopaji usalama na umiliki wa mali zao endapo watashindwa kulipa.” Ameeleza
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Bima kutoka Benki ya TCB, Francis Kaaya amesema Bima hizo ni kielelezo cha dhamira ya Benki ya TCB ya kuwasikiliza na kuwahudumia wateja kadri ya mahitaji yao na kuwahudumia watanzania kwa ujumla.
“Tunaelewa umuhimu mkubwa wa elimu katika kujenga kesho bora ya jamii yetu. Bima hii inawapa usalama wa kifedha, lakini pia inalea ndoto na matarajio ya wateja wetu.
Ameendelea kufafanua kuwa, “Bima hizi ni kielelezo cha dhamira ya TCB Benki ya kuwasikiliza na kuwahudumia wateja kadiri ya mahitaji yao na kuwahudumia Watanzania wote kwa ujumla.” Alieleza Kaaya
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Benki ya TCB, Jema Msuya amesema kama Taasisi za kifedha wanawajibu wa kumlinda mteja juu ya sintofahamu na majanga lakini pia wateja wao wanafikia ndoto zao bila wasiwasi.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Bima ya Metro Amani Boma amesema kupitia ushirikiano wao na Benki ya TCB wanajivunia kuwaletea watanzania huduma ya Bima kadri ya mahitaji yao lakini pia kuvisaidia vikundi vya huduma ndogo za fedha.
“Tunatambua mchango mkubwa unaofanywa na SACCOS pamoja na Vikundi vya huduma ndogo za fedha (micro-finance) katika kuimarisha uchumi na jamii yote nchini, kupitia ushirikiano wetu na TCB Benki tunajivunia kuwaletea Watanzania huduma ya bima kadiri ya mahitaji yao na pia kuvisaidia Vikundi vya huduma ndogo za fedha.”
Ushirikiano kati ya TCB Benki na Metro Life Assuarance ni mfano wa dhamira ya pamoja ya kuleta ubunifu ili kumridhisha mteja.
Taasisi hizi mbili zinakusudia kuleta mageuzi katika sekta ya bima ya benki hapa nchini kuelekea katika usalama wa kifedha na udhibiti wa biashara na mtu mmoja mmoja.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote