January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya NMB yapiga tafu Milioni 20 kinara wa ubunifu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Benki ya NMB imekabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Shilingi Milioni 20 kwa kinara wa Ubunifu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwa ni motisha kupitia mradi wa asili wa saruji inayotengenezwa kwa kutumia mabaki ya mimea na miamba.

Hundi hiyo ilikabidhiwa mwishoni mwa wiki hii Mei 26,2022 na Meneja Utafiti Masoko wa Benki ya NMB, Prochest Kachenje kwa Mpelelezi Mkuu wa Mradi huo, Dk Aldo Kitalika na kushuhudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Eliamani Sedoyeka.

Mradi huo unalenga kuzalisha saruji inayoweza kutumika mbadala ya saruji ya jadi na inatengenezwa kutokana na mabaki ya mimea na mabaki kutoka migodini kwa maana ya mawe na udongo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya hundi hiyo, Kachenje alieleza kuwa NMB imejidhatiti kuendelea kuchangia ukuaji wa utafiti na ubunifu.

“Kwa kuwekeza katika utafiti na uvumbuzi, tumechangia kwa kiasi kikubwa hatua ambazo nchi imepiga kwenye sekta ya kifedha na ukuaji wa uchumi kwa ujumla. Tutaendelea kubuni na kusambaza bidhaa za kidijitali zinazoendana na mahitaji ya wateja wetu na soko la Tanzania,” aliongezea Kachenje

Akipokea tuzo hiyo, Dk Aldo Kitalika aliishukuru benki hiyo kwa mchango wake na kusema fedha hizo zimepatikana wakati muafaka kwani tayari wameshaagiza mashine kutoka Uturuki yenye thamani ya Shilingi Milioni 47 na kutarajia kuanza uzalishaji Julai mwaka huu.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa, Eliamani Sedoyeka akimpongeza Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dk Aldo Kitalika baada ya kumkabidhi mfano wa Hundi ya Shilingi Milioni 20 katika Wiki ya maonyesho ya 7 ya Utafiti na Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam . Meneja Utafiti Masoko wa Benki ya NMB-Prochest Kachenje(wa pili kushoto) na Meneja mahusiano ya taasisi za umma na binafsi- Eliamani Kimaro(wa pili kulia)
Meneja Utafiti Masoko- Prochest Kachenje akizungumza na wanachuo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika maonyesho ya 7 ya Utafiti na Ubunifu.