Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Benki ya NMB leo wamekabidhi Sh. Bilioni 30.7 kwa Serikali huku Makamu wa Rais, Mhe.Dkt Philip Isdor Mpango akisema benki hiyo imefanya siku yake na Serikali nzima kuwa yenye furaha.
Makamu wa Rais alitoa kauli hiyo kufuatia agizo lake kwa benki hiyo mwaka jana kipindi kama hiki alipopokea gawio la Sh Bilioni 20.8 ikiwa ni faida ya 2020 na kutaka waongeze nguvu na ubunifu ili waje na gawio nono.
Gawio hilo limetolewa ikiwa ni faida ya NMB kwa mwaka wa fedha ulioishia 2021 ambapo jumla ya Sh. Bilioni 97 zilipitishwa na mkutano mkuu wa wana hisa wa Benki ya NMB kutolewa kwa wanahisa kama gawio.
Serikali ikiwa inamiliki hisa 31.8%, imepokea shilingi Bilioni 30.7 kama gawio lake kutoka benki ya NMB ikiwa ni ongezeko la 40% ukilinganisha na mwaka jana.
Kwa gawio hilo, Benki ya NMB ndani ya kipindi cha miaka mitano inakua imetoa jumla ya Sh. Bilioni 80.544 kwa Serikali.
Akipokea mfano wa hundi ya kiasi hicho, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango alisema benki hiyo imeendelea kuiheshimisha Serikali kwa kuonyesha namna gani inavyokuwa kimtaji na kuwajali wateja wake.
“Hata nitakapokwenda kumpokea Mheshimiwa Rais, hili litakuwa ni jambo la kwanza kumuambia, moyo wangu umeburudika sana, mmenifurahisha sana nasema hongereni sana,” alisema Dkt. Mpango.
Akitoa taarifa yake kwa Makamu wa Rais, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna alisema faida ya Benki baada ya kodi katika kipindi cha 2021 iliongezeka kwa asilimia 41 hadi kufikia Sh. Bilioni 290.
Kiasi hicho ni kikubwa ukilinganisha na Sh. Bilioni 206 ya mwaka 2020 ambapo idadi ya akaunti za wateja
iliongezeka hadi kufikia Milioni tano ikilinganishwa na milioni nne za 2020.
“Katika kuhakikisha Benki inaendelea kuwa na maendeleo endelevu, tumeweza kuongeza mtaji wa Benki hadi Sh. Trilioni 1.3 na iliendelea kuwa na ufanisi, na kuweka rekodi ya uwiano wa gharama za uendeshaji na mapato, kufikia asilimia 46,” alisema Zaipuna.
Zaipuna alisema kwa mwaka 2021, Benki ilipata Tuzo saba za kimataifa, ikiwemo ya benki bora nchini kwa mwaka wa tisa mfululizo ambayo iliyotolewa na Jarida la Kimataifa la Euromoney. Kwa mujibu wa Mtendaji huyo, hadi mwishoni mwa 2021, jumla ya mikopo ya Sh. Trilioni 4.3 ilikuwa imetolewa kwa wakulima, wafanyabiashara wadogowadogo, wa Kati na watu binafsi.
Akizungumzia mafanikio ya benki, alisema yalitokana na uwekezaji katika mifumo ya kidijitali, huduma za wakala, ambazo ziliongezeka na kufikia mawakala 10,194 ukilinganisha na 8,410 waliokuwepo 2020.
Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya NMB, Dkt. Edwin Mhede alisema gawio kwa mwaka wa 2022 wanatarajia kuwa na gawio nono zaidi kwani kwa kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo wamepata faida kubwa inayolingana na faida ya mwaka mzima katika kipindi cha miaka ya nyuma kutokana na ubunifu uliofanywa na watumishi wa benki.
More Stories
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi
Kampeni ya Sako kwa Bako yawafikia Kanda ya Kati