November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya NMB yaingia mtaani kuzungumza na wateja juu ya Teleza Kidijitali

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Benki ya NMB imeanza rasmi kampeni ya kuinadi Teleza Kidijitali iliyozinduliwa Aprili 11, 2022 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jijini Dodoma, na sasa ikipelekwa mtaani, kuwaelimisha Watanzania umuhimu wa huduma zilizo chini ya mwamvuli huo, ambazo ni NMB Pesa Wakala, Lipa Mkononi na Mshiko Fasta.

Kampeni hiyo imefanyika NMB Tawi la Tandika Wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, ambapo Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, akiambatana na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi na Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, kuzindua na kisha kuwatembelea wafanyabiashara madukani ili kuwapa elimu zaidi.

Akizungumza wakati ya uzinduzi huo, Zaipuna alisema ujio wake, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi, umelenga kutoa elimu ya kutosha na kuwaingiza Watanzania wengi zaidi kwenye Sekta rasmi ya Kifedha ili waweze kunufaika na huduma mbalimbali ambazo wanazitoa.

“Tuko hapa kunadi huduma zote muhimu zilizopo kwenye mwamvuli wa Teleza Kidijitali, ikiwa ni ufunguaji wa akaunti za NMB, Mshiko Fasta ambapo mteja anaweza kupata mikopo nafuu isiyo na dhamana kupitia simu yake tu.”

“Pia tumeutumia uzinduzi wa kampeni hii kwa ujumla kunadi huduma ya Lipa Mkononi, ambayo itamuwezesha mfanyabiashara kulipwa na wateja wake kwa kutumia lipa namba au kwa kuskani QR, huku ikitupa sisi kumbukumbu na historia ya mfanyabiashara huyo, kutusaidia hata katika utoaji wa mikopo.”

“Pia tumekuja na NMB Pesa Wakala, huduma inayomuwezesha mtu yeyote kuwa wakala kwa kupitia simu yako ya mkononi (smart phone au tochi) kutoa huduma za kuweka, kutoa au kutuma pesa kirahisi,” alisema Zaipuna, ambaye alishiriki kutembelea wafanyabiashara wa eneo la Tandika madukani mwao kutoa elimu na kusikiliza maoni yao.

Zaipuna aliielezea kampeni hiyo imelenga kuhakikisha Watanzania wanapata elimu ili waweze kuwa sehemu ya watumiaji wa huduma za sekta rasmi ya kifedha na huduma zao zinawafikia kiurahisi.Pia, anaamini suluhisho hizo zitakuwa chachu ya ukuaji kibiashara na kiuchumi kwa wateja wao kote nchini.

Kwa upande wake, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, aliwataka wakazi wa kanda yake kuchangamkia kampeni hii, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma bila kusumbuka kwenda matawini.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna(katikati), Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi(kulia) pamoja na Meneja wa NMB kanda ya Dar es salaam, Donatus Richard(kushoto) wakipeperusha bendera kama ishara ya Kampeni ya Teleza Kidijitali kuingia rasmi mtaani iliyofanyika NMB tawi la Tandika jijini Dar es salaam
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna akitoa elimu kwa mmoja wa wafanyabiashara Tandika, kuhusu Kampeni ya Teleza kidigitali yenye huduma ya NMB Pesa Wakala, Lipa Mkononi na Mshiko Fasta, iliyozinduliwa April 11, 2022 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Jijini Dodoma ambapo kwa sasa ipo mtaani.